Mradi wa kusafisha dhahabu kuanzishwa Mwanza
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Madini Doto Biteko akiieleza jambo Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini wakati wizara ilipowasilisha kwa kamati hiyo Taarifa kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya STAMICO kwa Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula akieleza jambo baada ya Wizara kuwasilisha kwa kamati hiyo Taarifa kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya STAMICO hilo kwa Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (mstari wa mbele) na Maafisa kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake wakifuatilia uwasilishaji wa Taarifa ya STAMICO kwa kamati hiyo.
Waziri wa Madini Doto Biteko akifafanua jambo anayefuatilia kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila pamoja na Watendaji wa Wizara na Taasisi na Wajumbe wa Bodi za Taasisi
Waziri wa Madini Doto Biteko akitoa ufafanuzi kwa kamati baada ya STAMICO kuwasilisha Taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Wanaofuatilia na baadhi ya wajumbe wa kamati na Maafisa wa Wizara.
Imeelezwa kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lipo katika hatua za awali za uanzishwaji wa Mradi wa Kusafisha Dhahabu (Gold Refinery) na tayari kampuni ya ubia ijulikanayo kama Mwanza Precious Metals Refinery Company Limited imeanzishwa.
Hayo yalibainishwa Januari 21, 2020 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa (STAMICO) Dkt. Venance Mwase wakati akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Taarifa kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya shirika hilo kwa Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa niaba ya Waziri wa Madini.
Dkt. Venance alieza kamati hiyo kuwa, mradi huo utaendeshwa kwa ubia ambapo STAMICO itakuwa na hisa asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75, huku ikilelezwa kwamba, mradi huo utakaojengwa jijini Mwanza utahusisha kujenga mtambo wenye uwezo wa kusafisha wastani wa kilo 200 hadi 500 kwa siku.
Aliongeza kuwa, makadirio ya fedha zinazohitajika ni Dola la Marekani Milioni 58.204 ambazo zimepangwa kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kusafishia dhahabu, gharama za awali za mradi, kununua dhahabu kutoka katika masoko pamoja na gharama zaza uendeshaji na kuongeza‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti tumepanga uwe mtambo wa viwango vya kimataifa,’’.
Aidha, Dkt. Mwase alisema kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019, tayari mradi umetekeleza majukumu kadhaa ikiwemo kupata leseni ya kujenga na kuendesha mtambo huo, kusainiwa mkataba wa ubia pamoja na kuanza taratibu za uanzishwaji wa kampuni ya ubia na kupata eneo la ujenzi wa mtambo chini EPZA.
Aliongeza majukumu mengine yaliyotekelezwa ni pamoja na kufanyika kwa Athari kwa Mazingira (EIA) kwenye eneo la mradi upembuzi yakinifu pamoja na kukusanya taarifa za upatikanaji wa dhahabu katika maeneo mbalimbali yanayokusudiwa.
Akizungumzia shughuli nyingine zinazoendeshwa na Shirika hilo alisema linaendelea kutoa huduma za kibiashara za uchorongaji miamba wa biashara katika sekta ya mafuta na gesi ambapo katika Mwaka wa Fedha 2019/20 ambapo limefanikiwa kupata kandarasi 4 za uchorongaji kupitia zabuni mbalimbali zenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 .
Kuhusu mgodi wa Stamigold ambao ni Kampuni Tanzu ya Shirika hilo aliieleza kamati hiyo kuwa, kuanzia Julai hadi |Desemba, 2019, mgodi huo umezalisha na kuuza wakia 7,133.00 za madini ya dhahabu na wakia 879.19 za madini ya fedha, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 24,172,700,255.34.
‘’Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hicho, mgodi umelipa jumla ya shilingi 1,712,455, 550.91 kwa ajili ya malipo ya mrabaha, ada ya ukaguzi na kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi,’’ alieleza Dkt. Venance.
Kuhusu mradi wa makaa ya mawe katika Mradi wa Kabulo na Kiwira, alisema jumla ya tani 4,359.10 ziliuzwa na kulipatia Shirika kiasi cha shilingi 17,558,184.76 na kuongeza kuwa, ‘’ shirika lilifanikiwa kulipa mrabaha, ada ya ukaguzi na tozo ya Halmashauri ya jumla ya shilingi 23,645,000.62.
Aidha aliongeza kuwa Mgodi umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 400.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na kamati, aliwatoa Hofu Wajumbe wa kamati hiyo kuhusu Maendeleo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo ameeleza pamoja na changamoto zinazolikabili, linakua na linafanya vizuri.
Waziri Biteko aliiomba Kamati hiyo kuendelea kuilea na kuishauri STAMICO kwa kuwa mwelekeo wake ni mzuri na kwamba hivi sasa lina uwezo wa kuzalisha hadi shilingi Bilioni 20 tofauti na ilivyokuwa awali na kuongeza kuwa, Watendaji na Bodi ya Shirika hilo mara zote wanafanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati pamoja na Wizara.
‘’Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa bahati mbaya sana kulifuta shirika hili. Linakua, wanaendelea vizuri na Wana Bodi nzuri, watendaji wanasikiliza ushauri na kuufanyia kazi na mapungufu yanafanyiwa kazi, naomba muendelee kuilea na kuishauri STAMICO,’’alisisitiza Waziri Biteko.
No comments: