LIVE STREAM ADS

Header Ads

Ukerewe yapigiwa chapuo kupata barabara za lami

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Judith Ferdinand, Mwanza
Imeelezwa kuwa Jimbo la Ukerewe lenye takribani kilomita 660 za mtandao wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Nchini (TARURA) halina hata km 1 ya kiwango cha lami kwa barabara zilizo chini ya wakala huo hivyo Serikali imeombwa kuliangalia suala hilo.

Hayo yalielezwa na Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Joseph Mkundi wakati akizungumza kwenye kikao cha pili cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kilichofanyika jijini hapa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza (RAS), Wabunge, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri na Watendaji wa Taasisi za Umma.

Mkundi alisema mbali na kukosa barabara za lami pia ata nyingine za udongo na changarawe ambazo zipo chini ya TARURA kimsingi kwa sasa zina hali mbaya hasa baada ya mvua kubwa kunyesha,miundombinu kwa ujumla kwenye barabara zao hazipo vizuri.

Aidha aliishukuru Serikali kwa kuwapatia milioni 50 kwa ajili ya jitihada za kurekebisha baadhi ya maeneo hasa kutokana na kuharibika na mvua zinazoendelea kunyesha,ambapo alisema,licha ya fedha hizo lakini bado wanahitaji msaada mkubwa, angalau barabara ziweze kupitika ikizingatiwa kwamba barabara hizo zilizo chini ya TARURA ndizo zinazogusa wananchi moja kwa moja kwani zinawasaidia kusafirisha mazao kutoka vijini kwenye mashamba kuja mjini kwenye masoko.

"Kimsingi jimbo letu la Ukerewe kwa upande wa Barabara tuna Mtandao wa barabara za Wilaya ya Ukerewe zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) takribani km 660 na bahati mbaya ni moja ya Wilaya kwa bahati mbaya haina hata km 1 ya barabara ya lami kwa barabara zilizo chini ya wakala,tumekuwa tukiendelea na jitihada mbalimbali angalau za kupata kilomita za lami,walau kuweza kupunguza shida za usafiri na usafirishaji katika eneo letu la Ukerewe" alisema Mkundi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TARURA kutoka Makao Makuu Mhandisi Abdul Digaga alisema kwa Mkoa wa Mwanza kweli kuna baadhi ya makao makuu ya wilaya zilizokuwa hazina barabara za lami maagizo ambayo yametoka wizara na Sera za kitaifa ni kwamba angalau mwaka huu kwenye makao makuu ya wilaya kuwe na hata barabara za lami mbili angalau za km 1.

"Hivyo kufuatia agizo hilo tumeanza kutekeleza ambapo ukiangalia takwimu zinaonyesha Wilaya ya Ukerewe,Buchosa,Kwimba na Misungwi hakuna lami zile tunazozisimamia sisi,tumeisha anza Kwimba na Misungwi hivyo tunategemea kufikia mwakani itakuwa Ukerewe na Buchosa" alisema Mhandisi Digaga.

Naye Mbunge wa Jimbo la Magu Boniventure Kiswaga alisema unaweza kuwa na mtandao mkubwa wa barabara ila fedha inayopatikana ni kidogo,aliwaomba Wabunge wenzie kusaidia hupatikanaji wa fedha ili miradi ya barabara iendelee huku akiomba barabara ya Airport, Kayenze hadi Magu itengenezwe kwa kiwango cha lami ili kupunguza msongamano.

Hata hivyo Ofisa Tarafa Mstaafu Mangabe Mnilago aliiomba TARURA kuweka vigingi( biconi) kwenye barabara ili Kuzuia wananchi kuvamia na kufanya shughuli kwenye barabara hizo huku Mbunge wa Jimbo la Sumve Richard Ndassa alisema, taa ziwekwe barabara ili wakati wa usiku ziwashwe na kutoa fursa ya wananchi kufanya biashara hadi nyakati za usiku sanjari na taasisi husika iombe pesa kwa ajili ya ujenzi wa mto Simiyu siyo wasubili likikatika ambapo alipendekeza ujenzi wa reli ya kati utakapo anza,uanzie Mwanza.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.