Wakazi wa Misungwi kupata huduma bora za Uzazi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Zaidi ya wakazi elfu sabini (wakazi 71,960)
hususani akina mama wajawazito na watoto katika Tarafa ya Mbarika Wilaya Misungwi
mkoani Mwanza, wanatarajia kunufaika na huduma bora za uzazi baada ya
kukamilika kwa ujenzi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Mbarika.
Hayo yalielezwa kwenye hafla ya
kukabidhi jengo la wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Mbarika lililojengwa
kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la nchini Canada (Global Affair) kupitia
mradi wa Mama na Mtoto uliokuwa unatekelezwa wilayani Misungwi kuanzia mwaka
2016.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya
Mbarika, Dkt. Barnabas Makanza alisema jengo hilo limegharimu shilingi Milioni
156 hadi kukamilika ambapo Shirika la Global Affair lilitoa shilingi Milioni
146, Halmashauri wa shilingi Milioni tano huku wanajamii wakichangia mawe,
mchanga pamoja na nguvu kazi ya kuchimba msingi
na maji na hivyo kufanya mchango wao kufikia thamani ya shilingi Milioni
tano.
Dk. Makanza alibainisha kwamba Jengo
hilo lina uwezo wa kuwekwa vitanda 31 vya kuhudumia wazazi wanne
kwa wakati mmoja pamoja na uwezo wa vitanda vinne vya kujifungulia (derivery
beds).
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa
Wilaya Misungwi Juma Sweda, Afisa Tawala Wilaya ya Misungwi Zubeda Kimario
aliwataka wananchi wa Tarafa ya Mbarika kuitunza vyema wodi hiyo ili kusaidia
mapambano dhidi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa
miaka mitano.
Naye Mganga Mkuu Wilaya ya Misungwi,
Dkt. Zabron Masatu alisema Tarafa ya Mbarika Wilayani Misungwi ni moja kati ya
maeneo yaliyokuwa yameshamiri vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka
mitano kutokana na adha ya kukosekana kwa
huduma za uzazi.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa mama
na mtoto, Tanya Salewski alisema mradi wa Mama na Mtoto umesaidia kuimarisha
huduma za uzazi kwa akina mama na watoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi
tangu mwaka 2016 na kufanikiwa kujenga jengo la upasuaji, kutoa gari la
wagonjwa (Ambulance) ambalo pamoja na ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje
katika Zahanati ya Nyamayinza na ukarabati wa chumba cha upasuaji mdogo katika
Zahanati ya Mwawile.
Kupitia Mradi wa Mama na Mtoto,
Halmashauri ya Wilaya Misungwi pia imepokea gari aina ya Toyati Nissan yenye thamani
ya shilingi Milioni 140 kwa ajili ya
kusaidia uboreshaji wa shughuli za afya wilayani humo.
Tazama BMG TV hapa chini
#BMGHabari
No comments: