LIVE STREAM ADS

Header Ads

Nyongo apiga marufuku vishoka "amsimamisha Mkaguzi wa Madini"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (pichani) amepiga marufuku watu wanaofanya biashara nje ya mfumo wa masoko yaliyoanzishwa maarufu kama vishoka na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo Juni 29, 2020 kwenye mkutano wake na wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini Tunduru ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye soko hilo yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye uendeshaji wa soko hilo.

Alisema katika Soko la Madini la Tunduru wapo watu wasio waaminifu wamekuwa wakifanya biashara ya madini nje ya soko la madini lililoanzishwa na kuongeza kuwa Serikali haitawafumbia macho kwa kuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi kutokana na kukwepa kodi mbalimbali zinazotakiwa kulipwa Serikalini.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inakuja na mkakati mpya wa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa madini wanatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa.

Katika hatua nyingine Nyongo alisema kuwa ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wananufaika na shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliamua kufuta kodi nyingi zilizokuwa kero kwa wachimbaji wa madini pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini.

Nyongo aliwataka maafisa madini wakazi nchini kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama na Taasisi nyingine za Serikali.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Nyongo alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkaguzi Msaidizi wa Madini, Athumani Masawe ambaye alituhumiwa na wanunuzi wa madini kuhusika na kufanya biashara nje ya soko kinyume na sheria ya madini.

Aidha aLIkemea vikali tabia ya viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Wilaya ya Tunduru kuingilia shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini ndani ya Soko la Madini la Tunduru.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alimpongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kufanya ziara kwenye soko hilo na kutatua changamoto zilizojitokeza na kuongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma kwenye usimamizi wa Soko la Madini Tunduru ili liwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.
Na Greyson Mwase, Tunduru

No comments:

Powered by Blogger.