LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mongella afungua Kongamano la waalimu jijini Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella amefungua kongamano la ujirani mwema la Chama cha Waalimu Tanzania (CWT) kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Kigoma, Kagera na Geita linalofanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 03, 2020 jijini Mwanza.

Akifungua kongamano hilo, Mongella aliwapongeza waalimu kwa mabadiliko makubwa ya kiutendaji waliyoyafanya kupitia chama chao hatua ambayo imeondoa malalamiko mbalimbali yaliyokuwa yakiwakabili.

Aidha Mongella alibainisha kuwa uwajibikaji wa waalimu pia umechochea kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi akitolea mfano Mkoa wa Mwanza ambao kwenye matokeo ya kidato cha sita wamepunguza daraja sifuri kutoka 49 mwaka uliopita hadi tisa mwaka huu.

Katika hatua nyingine Mongella alisisitiza kuwa watumishi wa umma wa ngazi mbalimbali wakiwemo waalimu walioshiriki mchakato wa Uchaguzi Mkuu na kutofanikiwa kuchaguliwa wanapaswa kurejea kazini bila masharti, wakiwa na stahiki zao zote kama alivyoagiza Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

"Walitakiwa kuwa wamerudi maofisi tangu juma lililopita, sasa kwenye Mkoa wangu kuna baadhi ya maeneo watu bado wana kigugumizi, haya ni maelekezo mahususi ya Rais, wanarudi kazini wakiwa na haki zao zote" alisisitiza Mongella.

Naye Rais wa CWT, Mwl. Leah Ulaya alihimiza mshikamano miongoni mwa waalimu na kwamba watakuwa mabalozi wazuri wa kuhakikisha amani, utulivu, utu wema na ulinzi vinaimarishwa katika kipindi chote cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.

Awali Katibu wa CWT Mkoa Mwanza, Mwl. Daudi Mafwili alisema kongamano hilo linalenga kuwajengea uwezo waalimu kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo sheria za utumishi, mfuko wa fidia kwa wafanyakazi, ujasiriamali, benki ya waalimu, ushirikishwaji wa waalimu kwenye vikao (DCC na RCC) na mabaraza ya halmashauri, historia, mafanikio na changamoto za CWT.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

No comments:

Powered by Blogger.