Watu 12 mbaroni kwa tuhuma za utapeli na kuchana mabango ya wagombea
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Watu 12 wakiwemo wanne wanaotuhumiwa kujihusisha na utapeli wa kimataifa katika taasisi mbalimbali za fedha (benki), wanashikiliwa na polisi mkoani Mwanza kwa makosa ya utapeli na kuchana mabango ya wagombea Ubunge na udiwani jijini Mwanza.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao wa utapeli akiwemo raia mmoja wa nchini Uganda, Rutayisere Patrick Mande (38), walikamatwa Septemba 6 saa 5:00 adhuhuri jijini hapa wakiwa katika harakati za kufanya utapeli kwa kutumia fedha za kigeni (dola za kimarekani) na za kitanzania.
Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na raia huyo wa Uganda ambapo walikutwa na Dola 192 za Marekani sawa na sh 441,000 na fedha taslimu za kitanzania sh 127,000 ni pamoja na Yelemi Mussa maarufu kama Badru (45) dereva na mkazi wa Tuwangoma jijini Dae es salaam.
Wengine ni Mussa Juma (44) mfanyabiashara wa matofali na mkazi wa Shamba Muleba mkoani Kagera na mwanamke mmoja Delphina Kungu (51) mkulima na mkazi wa Ilongero mkoani Singida.
"Pamoja na fedha hizo za kigeni na kitanzania, vilevile walikamatwa wakiwa na makalatasi yaliyokatwa mithili ya noti yakiwa yamefungwa kwa pamoja na fedha hizo na kuwekwa kwenye bahasha" alisema Muliro na kuongeza kuwa walikamatwa na gari lenye namba za usajiri T.205 BGW aina ya Chaser yenye rangi nyeupe.
Alisema baada ya kuhojiwa kwa kina walikiri kujihusisha na matukio ya utapeli katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar, Mbeya, Arusha, Kigoma, Tanga na katika baadhi ya nchi jirani za Uganda, Zambia na Kenya.
"Mbinu wanazotumia matapeli hao ni kwenda kwenye ndani ya mabenki na kujifanya hawana uelewa wa taratibu za kubadilisha fedha za kigeni ambapo hutaja kiwango cha chini cha ubadilishaji Dola za kimarekani na kuomba msaada kwa mteja wanayemlenga baada ya kubaini ana fedha" alisema.
Kamanda huyo alifafanua kuwa mteja huyo akikubali kuwasaidia na kuingiwa tama ya kujipatia faida kirahisi kupitia kwao, wanamrubuni na kutoka naye nje ya Benki na kwenda sehemu nyingine ikiwemo hotelini ambapo hutapeliwa kwa kupewa fedha zenye thamani ndogo na makalatasi hayo.
Katika matukio mengine yaliyotokea kwa nyakati tofauti wiki hii jijini Mwanza, jeshi la polisi pia liliwakamatwa watu wanane kwa tuhuma za kuchana mabango ya wagombea wa nafasi mbalimbali za udiwani na ubunge wilayani Nyamagana jijini hapa.
Muliro alisema kwamba watuhumiwa hao walichana mabango ya wagombea udiwani na ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye maeneo tofauti wilayani Nyamagana kitendo ambacho kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ni kosa la jinai.
Kamanda huyo aliwataja watuhumiwa hao ambao wanne kati yao wamefikishwa mahakamani kuwa ni Masalu Bululu (24) Kondakta wa Daladala, John Juma (20) na Stephen Augustine (22) wakazi wa Igoma jijini Mwanza, Amani Stephano (33) mkazi wa Bugalika Mwanza na Abuu Abubakary (28) mkazi wa Kanyerere Mahina wilayani Nyamagana.
Wengine ni Samuel Matongo (32) mkazi wa Bugarika Mwanza, Seleman Issa (25) mkazi wa Butimba Mwanza na Abas Gerald (33) mkazi wa Malimbe ambaye upelelezi wa tuhuma zinazomkabili unaendelea.
No comments: