LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanafunzi Iseni Mwanza wapanda miti kuadhimisha Siku ya Mazingira

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Jumla ya miti 1030 imepandwa katika Shule ya Msingi Iseni B ya jijini Mwanza zikiwa ni jitihada za kuhifadhi mazingira katika Shule hiyo ambayo inakabiliwa na upungufu mkubwa miti.

Akizungumza Juni 05, 2021 katika zoezi hilo la upandaji miti lililoandaliwa na Shirika la Usimamizi wa Mzingira na Maendeleo (EMEDO), Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Donald Chakachaka Jovine alilishukuru shirika hilo kwa kuendelea kuisaidia Shule hiyo katika suala zima la mazingira.

Alisema hii ni mara pili kwa shirika hilo kutoa miche ya miti ambapo awamu ya kwanza waliota miche 1,000 ambayo ilipandwa yote na safari hii ya pili kuelekea siku ya Mzingira Duniani wametoa miche 1,030 ya miti inayohimiri ukame kwa ajili ya kuhifadhi mazingira katika shule hiyo.

"EMEDO wamekuwa msaada mkubwa kwetu kwanza wamefufua Klabu ya Mazingira ambayo ilikuwa imekufa na sasa ipo imara na wanachama wake ni kuanzia Darasa la Awali hadi darasa la Sita na kwakweli watoto wanafanyakazi kubwa katika suala la mazingira ya shule" alisema Mwalimu Chakachaka.

Akizungumzia sababu za kuwaingiza watoto wa darasa la awali ambao wengi wao wana umri wa miaka mtatu, minne hadi mitano Mwalimu Chakachaka alisema walifikia uamuzi huo ili kuanza kuwajenga watoto kujua umuhimu wa utunzaji wa mazingira na watakuwa mabalozi wazuri kwa siku zijazo.

Editrudith Lukanga ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la EMEDO aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanahifadhi mazingira ili nayo yaje yawatunze na kuwasisitiza kutojali kuhusiana na umri wao kuwa mdogo kwani wanaweza kufanya mambo makubwa katika mazingira katika umri huo huo walionao.

Alimtolea mfano Mratibu wa Shirika la Flip Flop, Mliha Sumari ambae kiumri ni mdogo lakini kapewa jukumu kubwa la kuendesha shirika kubwa la mazingira ambalo linapambana na taka za plastiki.

Naye Mwakilishi wa Shirika la British Council Tanzania, Ephraim Kapungu aliwapongeza watoto wa darasa la awali ambao nao ni wanamazingira pia na kuongeza kuwa ameambiwa wamekuwa watunzaji mazingira na watumiaji wazuri wa vyoo hali inayopelekea kuepuka magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake Mwanachama wa Klub ya Mazingira shuleni hapo kutoka darasa la awali Mabula Fransis (4) alishukuru shirika la EMEDO na kuwataka kuendelea kuwafadhili katika mahitaji yao ya kuhakikisha mazingira ya shuleni hapo yanakuwa bora na kuahidi kushinda katika shindano la mazingira ambalo limeandaliwa na Waziri Ofisi ya Mkamu wa Rais Mazingira.

Oswald Mpelasoka ambaye ni Afisa Afya na Mazingira jiji la Mwanza aliwakumbusha wanafunzi kuwa suala la mazingira na afya ni vitu vinavyokwenda pamoja na kuwataka kuihimiza jamii kuhifadhi vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji ili kuvilinda vyanzo hivyo pamoja na kuhakikisha maji yanakuwa safi kwa matumizi ya binadamu.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka Juni 05 ambapo kitaifa maadhimisho hayo mwaka huu 2021 yalifanyika mkoani Dodoma yakiwa na kauli mbiu inayosisitiza kuirudisha Dunia katika mfumo wa Ekolojia.
Na Tonny Alphonnce, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.