LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWANZA: Kalemani azindua Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amemtaka mkandarasi kampuni ya Sengerema Engineering Group kuhakikisha anasambaza umeme katika Vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo katika Wilaya Magu mkoani Mwanza.

Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo Julai 19, 2021 katika Kijiji cha Isolo wilayani Magu wakati akizindua mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA) Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili huku akiongeza kuwa mradi huo haupaswi kuacha Kijiji hata kimoja.

Aidha Dkt. Kalemani alitoa muda wa siku 30 mkandarasi huyo ahakikishe anafikisha umeme katika Vijiji vingine wilayani Magu kuanzia Nyasato, Ngaya, Jinjimili, Ndalo na Mahaha na kwamba wananchi hawapaswi kulipa gharama zaidi tofauti na iliyoelekezwa na Serikali ambayo ni shilingi elfu 27 tu.

"Pia Vitongoji vya Kijiji hiki cha Isolo kuanzia  Isolo juu, Ngwandudu, Cheyo na Mwenezi lazima vipate umeme hadi kufikia Agosti 30 mwaka huu" alisisitiza Dkt. Kalemani huku akiwahimiza wananchi kuitumia vyema miradi hiyo kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwemo viwanda vidogo.

Aidha Dkt. Kalemani alibainisha kuwa tayari Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 42.6 kwa ajili ya kusambaza nishati ya umeme katika Vijiji zaidi ya 100 mkoani Mwanza na kwamba tayari Vijiji 541 tayari vimefikishiwa huduma hiyo.

Katika hatua nyingine Dkt. Kalemani alieleza hadi kufikia Disemba mwakani 2022, Serikali inatarajia kufikisha umeme katika Vijiji 12,268 ambavyo havijafikiwa na nishati hiyo kote nchini na kuwataka wakandarasi kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati.

Naye Meneja wa REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale alisema Vijiji 57 vitafikiwa na nishati ya umeme katika Wilaya Kwimba, Magu Vijiji 37 na Vijiji saba wilayani Sengerema. Alibainisha kuwa katika Wilaya ya Magu pekee Serikali imetenga shilingi bilioni 10.8 kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo huku shilingi milioni 889 zikitumika katika Kijiji cha Isolo ulipofanyika uzinduzi wa mradi huo.
#BMGHabari
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alizindua kituo cha umeme katika mgodi wa 'Busolwa Mining Group' uliopo Wilayani Misungwi na kuipongeza TANESCO kwa kazi nzuri waliyofanya.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.