LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watoto mkoani Tabora hatarini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Watoto wanaoishi katika Kijiji cha Chanhamagumo Kata ya Semembela Wilaya Nzega mkoani Tabora wapo hatarini kupatwa na magonjwa ya Nyongeza na Marasmus (kwashakoo) kwa wakati mmoja kutokana na kukosa lishe bora.

Hatari hiyo inatokana na Kijiji hicho kukabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa chakula cha kutosha kwa baadhi Kaya pamoja na kupanda kwa gharama za maisha kunakosababisha baadhi ya Kaya kushindwa kumudu hata mlo mmoja wa siku.

Magonjwa hayo huwapata watoto wanaonyonya wenye umri wa kati ya miezi sita hadi 18 ambao hawanyonyi vizuri kutokana na mama kukosa mlo kamili hususani vyakula vinavyoongeza maziwa.

Watoto wengine wenye hatari ya kupata magonjwa hayo ni wale waonyonyeshwa maziwa ya chupa, waliotelekezwa au kulelewa na wazee, wasiopata mlo kamili na wanaougua mara kwa mara.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chanhamagumo, Jumanne Pambe alisema hali ya maisha ya wanakijiji wengi ni mbaya kutokana na kutegemea kilimo ambacho kwa sasa hakifanyi vizuri kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Hivi sasa wanakijiji wanalima lakini hawapati chakula cha kutosha kutokana na ardhi kuchoka na kupoteza rutuba na wengi wanaendelea kulima bila kutumia mbolea kutokana na kuuzwa kwa gharama kubwa" alisema Pambe.

Naye Nhonge Maganga ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho mwenye mke na watoto wadogo wawili alisema familia yake inapitia kipindi kigumu kutokana na kukosa mahitaji muhimu kikiwemo chakula.

Maganga alisema mwaka jana alijaribu kulima lakini hakupata mazao ya kutosha kutokana na ardhi kuchoka.

"Hali ni mbaya tunaiomba Serikali iangalie namna ya kutusaidia chakula, watoto wangu wanaugua mara kwa mara, nadhani ni kutokana na kula chakula cha aina moja na mbaya zaidi hakiwatoshelezi" alisema Maganga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Matata, Izunya aliiomba Serikali kuwasaidia wakulima waweze kupata mbolea kwa bei nafuu ili waweze kuzalisha mazao kwa wingi kama zamani hali itakayowasaidia kupata mavuno ya kutosha na kuuza ziada kwa ajili ya kupata kipato cha kujikimu.

Izunya alisema pamoja na wakulima kusaidiwa pembejeo, Serikali pia inatakiwa kuikarabati barabara ya Kijiji hicho cha Chanhamagumo ili magari yaweze kufika kijijini hapo hasa wakati wa mavuno na kubeba mazao ambayo yataenda kuuzwa mjini na kuwaongezea kipato wanakijiji.

Joseph Nkuba ambaye ni Bwana Shamba alisema hali ya wanakijiji hao si nzuri na kutoa rai kwa Serikali kuweka ruzuku kwenye pembejeo zote na kuziuza kwa hati punguzo hasa upande wa Kaya masikini.

Nkuba alisema pia kuna ulazima Serikali kuhakikisha inawapatia usafiri wa uhakika Mabwana Shamba ili waweze kuwafikia na kuwasaidia wakulima kwa ukaribu ili walime kwa tija na kuinua kipato chao.
Na Tonny Alphonce, Nzega Tabora

No comments:

Powered by Blogger.