LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mradi wa kuhamasisha Amani wazinduliwa Tanzania

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mradi wa "Mtandao wa Vijana wa Nchi za Maziwa Makuu kuhusu Amani na Usalama" unaolenga kuhamasisha utunzaji amani katika nchi za Maziwa Makuu umezinduliwa nchini Tanzania huku vijana wakihimizwa kuwa chachu ya amani katika nchi hizo.

Mradi huo (Great Lakes Youth Network for Dialogue and Peace) ulizinduliwa Juni 30, 2021 katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza ambapo Tanzania imekuwa nchi ya pili kuzindua mradi huo ikitanguliwa na Uganda na baadae utazinduliwa DRC Congo, Burundi pamoja na Rwanda.

Katika hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa Mwanza, Eng. Robert Gabriel iliyosomwa na Mstahiki Meya wa Manispaaa ya Ilemela, Renatus Mulunga ilielezwa kuwa duniani kote kuna takribani vijana bilioni 1.8 ambapo kati ya hao, vijana milioni 600 wanaishi katika maeneo ama nchi zenye migogoro.

"Mkawe mabalozi wa amani na utulivu huku mkiifanya kazi hii ya kuchochea amani kwa weledi, uzalendo na wivu mkubwa kwa Taifa lenu na nchi za Maziwa Makuu" alisisitiza Mulunga akisoma hotuba hiyo ya ufunguzi.

Naye Meneja wa Mradi huo, Mariam Kagazi alisema vijana watakuwa na mchango mkubwa wa kuleta amani na utulivu katika mataifa yao kwani wengi wao wamekuwa wakiathirika kutokana na machafuko ama migogoro mbalimbali ikiwemo vita kutokana na kudhaniwa kuwa wao ndio chanzo.

Kwa Tanzania, mradi huo unajumuisha taasisi zaidi ya 20 kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Kagera, Geita na Kigoma ambapo utatoa fursa kwa vijana kujadili na kuzitafutia utatuzi changamoto wanazokumbana nazo Bila kujali itikazi zao.
#BMGHabari
Mstahiki Meya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga akizungumza kwenye uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel.
Mkurugenzi wa Shirika la Konrad Adenauer Stiftung(KAS), Tilmann Feltes akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mtandao wa Vijana wa Maziwa Makuu kuhusu Midahalo na Amani, uliofanyika jijini Mwanza.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Demokrasia na Utawala Bora (ADLG), Jimmy Luhende akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia uzinduzi huo.
Washiriki wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Mradi huo (Great Lakes Youth Network for Dialogue and Peace) unafadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (European Union). Wadau wengine ni Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) la Ujerumani pamoja na Actions for Democrancy and Local Government (ADLG) kutoka Tanzania.
Picha na Michael Jamson, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.