LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la Reli (TRC) laendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mradi wa SGR Mwanza-Isaka

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Afisa Mwandamizi, Kitengo cha Ardhi TRC, Fredrick Kusekwa akizungumzia masuala ya Thamini na Fidia katika mkutano wa kampeni ya Uelewa kwa Jamii kuhusu mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) uliofanyika katika Kijiji cha Fela wilayani Misungwi, Julai 10, 2021.
Mtaalamu kutoka katika Kitengo cha Ulinzi na Usalama wa Reli TRC, Mussa Mhagama akionesha moja kati ya alama za tahadhari zitakazowekwa katika eneo la mradi wakati wa kampeni ya Uelewa kwa Jamii kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Mwanza- Isaka iliyofanyika Kijiji cha Ibogoya "A" Kata ya Kolomije wilayani Misungwi.
Meneja Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Mwanza-Isaka, Mhandisi Mchibya Masanja akielezea lengo la kampeni ya Uelewa Kuhusu Mradi wa SGR Mwanza- Isaka katika Mkutano na wanakijiji wa Ibogoya "A" Kata ya Kolomije wilayani Misungwi.


Na Mwandishi Maalum, Mwanza
Shirika la Reli Tanzania- TRC linaendelea na kampeni maalum ya utoaji wa elimu juu ya ujenzi wa
Reli ya kisasa (SGR) awamu ya kwanza kipande cha tano kutoka Fela Mwanza hadi Isaka Shinyanga (Km 341) kwa jamii zinazoishi maeneo yatakayopitiwa na mradi.

Kampeni hiyo ya uelewa wa jamii kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR Mwanza – Isaka ilianza tarehe 28 Juni 2021 katika Mkoa wa Mwanza kwa timu ya Mawasiliano kutoka TRC kuzungumza na viongozi wa ngazi ya Wilaya mpaka Kata katika Wilaya za Kwimba, Misungwi na Nyamagana na baadaye kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi.

Lengo la kampeni hii endelevu ni kuhakikisha uelewa sahihi wa masuala yanayohusiana na mradi kwa viongozi na wananchi kwa ujumla ili kufikia maendeleo ambapo ni moja kati ya hatua muhimu za awali za utekelezaji wa mradi.

"Mradi huu ni shirikishi, kwahiyo tunafanya kampeni hii ili kuhakikisha mradi unakuwa na tija kwa wanachi ambao ndio walipakodi zinazotumika katika utekelezaji huu.Tunataka mradi ubadilishe maisha ya watu kwa kuwaletea maendeleo" alisema Meneja Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa SGR Kipande cha Mwanza – Isaka, Mhandisi Machibya Masanja, wakati akitoa ufafanuzi wa kampeni hiyo katika moja ya mikutano ya hadhara na wanamwanza.

Kampeni hii endelevu inayohusisha wataalam kutoka TRC vitengo vya Uhandisi, Ardhi, Habari na Mawasiliano, Mazingira, Ulinzi na Usalama wa Reli pamoja na kitengo cha Masuala ya Kijamii, tayari imekwisha wafikia wananchi kupitia mikutano ya hadhara katika Kata za Malya, Mwandu na Mantale Wilayani Kwimba na Ukiriguru, Mamaye na Kolomije za wilayani Misungwi.

Katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Kata hizo, wananchi wamejitokeza kwa wingi ambapo pamoja na kupata maelezo ya kina kuhusu mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) wananchi hao wameeleza jinsi ambavyo wameipokea kampeni ya uelewa kuhusu mradi huu wa kimkakati na kihistoria kwa taifa.

"Elimu hii itatusaidia sana hasa sisi vijana, maana fursa ni nyingi kutokana na mradi huu kwahiyo elimu hii iatatusaidia kuzitambua zaidi lakini pia tunaahidi kuulinda mradi" alisema Mathias Nyama, mkazi wa Kijiji cha Kitunga, Kata ya Malya wilayani Kwimba.

Kwa upande wake Neema Joseph, mkazi wa Kijiji cha Magaka, Kata ya Mamaye wilayani Misungwi alieleza kuwa kupitia mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), anaishukuru Serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati unaolenga kuwanufaisha watanzania.

Awali akizindua rasmi kampeni ya Uelewa wa Jamii kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Mwanza – Isaka, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi aliwahakikishia wanamwanza na Kanda ya Ziwa kuwa wananchi wote watakaopitiwa na huo watalipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Aidha katika awamu hii, kampeni ya uelewa wa jamii Kuhusu mradi wa SGR Mwanza – Isaka, inategemea kuwafikia viongozi na wananchi wa mikoa ya Simiyu na Shinyanga ambayo pia inapitiwa na kipande cha tano cha mradi huo (Mwanza – Isaka) utakaogharimu kiasi cha Sh. Trilioni 3.0617 za kitanzania.

Mbali na vikao vya ndani na viongozi na mikutano ya hadhara na wananchi, timu ya Mawasiliano kutoka Shirika la Reli Tanzania, vilevile inaendelea kutoa elimu kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyoko mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi nzima.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.