LIVE STREAM ADS

Header Ads

TAMWA yawataka Wanahabari kuvunja ukimya

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimekemea vikali suala la ukatili na unyanyasi wa kingono hususani kwa wanawake na vijana katika vyombo vya habari na kutaka wanahabari wenyewe kuvunja ukimya kwa kuripoti vitendo hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben aliyasema hayo hivi karibuni wakati akifungua mafunzo kwa wanahabari mkoani Morogoro, yaliyolengwa kuwajengea uwezo ili kupambana na ukatili wa kingono katika vyumba vya habari.

Dkt. Reuben alisema “hatutaacha kujifunza, tukiacha hatutaweza kubadili matatizo ya ukatili wa kijinsia ikiwemo wa kingono katika vyombo vya habari na jamii nzima hivyo baada ya mafunzo haya mkawe chachu ya mabadiliko katika vyombo vyenu vya habari".

Aidha Dkt. Reuben alisisitiza kuwa lazima wanahabari wenyewe wakavunja ukimya kwa kuripoti vitendo vya ukatili wa kingono kuanzia kwenye vyombo vyao vya habari badala ya kuwa mstari wa mbele kulipoti vitendo vya aina hiyo vinavyotokea nje ya vituo vyao vya kazi.

"Lazima tuvunje ukimya, tukivunja ukimya suala hili litaisha katika vyombo vya habari hadi kwenye jamii" alisisitiza Dkt. Reuben huku akibainisha kuwa tatizo la ukatili wa kingono katika vyombo vya habari nchini Tanzania ni kubwa.

Nao washiriki wa mafunzo hayo walisema watayatumia vyema kwa kufanya kazi kwa weledi ili kufichua vitendo vya unyanyasi na ukatili wa kingono katika vyombo vya habari pamoja na jamii inayowazunguka.

“Wanawake wanakumbana na changamoto nyingi, mafunzo haya yatatusaidia kuandika habari kwa usahihi na kufichua maovu yanayotendeka katika vyombo vyetu vya habari" alieleza Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Morogo (MOROPC), Lilian Kasenene.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoambatana na mdahalo wa siku moja uliolenga kujadili hali ya ukatili wa kingono katika vyombo vya habari ambapo ilielezwa kuwa waandishi wa habari wanawake walio kazini, wanaoomba kazi na wale wanaofanya mafunzo kwa vitendo wanakumbana na vitendo vya ukatili wa kiongono kutoka kwa wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari lakini wananyamazia vitendo hivyo.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji TAMWA, Dkt. Rose Reuben akifungua mafunzo hayo.
Mkurugenzi Mtendaji TAMWA, Dkt. Rose Reuben alisema chama hicho kinashirikiana na taasisi mbalimbali za kihabari kutekeleza mradi wa kuwawezesha waandishi wa habari wanawake na vijana kuvunja ukimya na kufichua vitendo vya ukatili wa kingono katika vyumba vya habari ukifadhiliwa na taasisi ya IMS.
Afisa Programu kutoka TAMWA, John Ambrose aliwahimiza washiriki wa mafunzo hayo yaliyowashirikisha pia waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Singida na Mwanza kuyatumia vyema ili kuletamabadiliko yaliyokusudiwa.
Washiriki wa mafunzo hayo wakieleza hali ya ukatili wa kingono ilivyo katika vyombo vyao vya habari.
Washiriki wakimsikiliza mshiriki mwenzao, Merina Makasi kutoka Ngasa TV Online (kulia).
Washiriki wakiwa kwenye majadiliano kupitia makundi.
Washiriki wa mafunzo hayo wakijadiliana na kutoa mapendekezo nini kifanyike ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kingono katika vyombo vya habari.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa kwenye majadiliano.
Washiriki wa mafunzo hayo walisema mabadiliko ya kisera katika vyombo vya habari pia yatasaidia kupambana na ukatili wa kijinsia wakisema kila chombo cha habari lazima kiwe na sera inayozuia ukatili wa kingono kazini.
Mshiriki Esther Baraka kutoka Afya Redio ya jijini Mwanza akitafakari wakati wa kila mshiriki kuandaa mapendekezo na mikakati ya kupambana na ukatili wa kingono katika vyombo vya habari.
Washiriki wa mafunzo hayo walikubaliana kuvunja ukimya kwa kuripoti matukio ya vitendo vya ukatili wa kingono katika vyombo vya habari.
Afisa Habari kutoka TAMWA akiendelea kunasa matukio.
Mkurugenzi TAMWA, Dkt. Rose Reuben (kushoto) na Katibu wa MOROPC, Lilian Kasenene (kulia) wakihesabu kura za washiriki ambapo kundi la wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari lilipata kadi nyingi nyekundu ikiwa ni ishara kwamba ndilo kundi hatari zaidi kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kingono katika vyombo vya habari.

No comments:

Powered by Blogger.