Siku ya Marafiki Duniani, watoto wapewe nafasi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuwapa nafasi watoto wao ya kuwa na marafiki ili waweze kukua haraka kiakili pamoja na kuwaondolea tatizo la upweke ambalo huwakumba watoto wengi duniani wanaofungiwa ndani.
Mbobezi wa masuala ya Ukunga na Afya ya Mama, Dkt. Denis Kashaija ameyasema hayo wakati akiizungumzia Siku ya Marafiki Duniani ambayo huadhimishwa Julai 30 kila mwaka kote duniani.
Dkt. Kashaija anasema kwa miaka ya hivi karibuni, malezi kwa watoto yamekuwa ni changamoto kubwa kutokana na watoto kuwa na maadui wengi hali ambayo imewafanya wazazi kuwajengea watoto uzio flani kwenye familia ili wasiweze kuingiliana na watoto wengine kwa lengo la kuwalinda wasifanyiwe vitendo viovu kitu ambacho kinawanyima watoto uhuru wa kuwa na marafiki.
Aidha anabainisha kuwa wazazi wengi hivi sasa wamekuwa na tabia ya kuwabana watoto kwa kuwafungiwa ndani na kuwawekea katuni kwenye luninga (TV) ama kuwawekea michezo ya ndani na wakitoka nje kucheza wazazi wanahakikisha wapo karibu jambo ambalo ni zuri lakini kiuhalisia wazazi hawana muda wa kuwa karibu na watoto wao muda wote wanapotaka kucheza na wenzao.
"Pamoja na changamoto zote, wazazi wanatakiwa kujua mtoto mwenye umri wa kuanzia mwaka mmoja na nusu anahitaji marafiki ambao ni watoto wenzake kwa sababu mtoto katika umri huo akiwaona wenzake anafurahi na kadri anavyokua anaanza kuwaiga wenzake kuongea au michezo wanayocheza na hii husaidia mtoto kuongea mapema na hata kuanza kutembea mapema kutokana na kuwaiga wenzie kile wanachofanya" alisema Dkt. Kashaija.
Kwa upande wake Dkt. Gema Simbee ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando anasema mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka minne ni vyema akawa huru kuchagua rafiki wa kucheza naye shuleni na hata nyumbani ambapo mzazi jukumu lake ni kumsaidia kuchagua marafiki wema.
Dkt. Gema anasema mzazi pia anaweza kujipa muda wa kuchunguza tabia za marafiki aliowachagua mtoto na akiona tofauti amshauri kuhusu marafiki hao endapo ataona sio marafiki wazuri kwake.
Anasema watoto hufurahi zaidi wanapokuwa na marafiki zao na hii hujionyesha pale mzazi anapompa zawadi mtoto ambapo hujisikia vizuri wanapoweza kuzitumia zawadi hizo pamoja na marafiki japo kuwa wakati mwingine huweza kugombana kutokana na kugombania zawadi hizo.
Naye Mwalimu Christina Wanchoke kutoka Shule ya Msingi Nyegezi ya jijini Mwanza, kitengo cha watoto wenye mahitaji maalum anasema urafiki unawasaidia watoto shuleni hasa upande wa masomo ambapo usaidiana na kupata matokeo mazuri darasani.
Anasema Walimu wanasisitiza urafiki kwa wanafunzi na ndio maana vikundi (Clubs) mbalimbali zinaundwa mashuleni zikiwemo za masomo, mazingira na ushauri nasaha ambapo mrengo wake ni kuwaunganisha wanafunzi pamoja kwa lengo la kuwasaidia kuona umuhimu wa kushirikiana katika mambo mbalimbali.
Siku ya Marafiki imelenga kusherehekea urafiki duniani ambapo ilianzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa mwaka 1958. Hapo awali ilikuzwa na tasnia ya kadi za salamu lakini baadae ikahamia katika mitandao ya kijamii ambapo nchi za India, Bangladesh na Malaysia zilitajwa kuongoza.
Mwaka 2011 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasimi siku hii ya urafiki duniani ili kuhamasisha amani katika nchi mbalimbali duniani na kujenga mahusiano mazuri kati ya jamii moja na nyingine.
Na Tonny Alphonce, Mwanza
No comments: