LIVE STREAM ADS

Header Ads

Jamii yapewa angalizo ugonjwa wa afya ya akili

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Imeelezwa kuwa watoto kushindwa kujisaidia haja ndogo na kubwa (kujisaidia kwenye nguo) ni miongoni mwa dalili za ugonjwa wa afya ya akili hivyo wazazi ama walezi wanapoona dalili hizo ni vyema wakawasaidia watoto wao kupata matibabu mapema.

Hayo yalielezwa Oktoba 07, 2021 na Daktari Bingwa wa Watoto na Vijana Dkt. Gema Simbele wakati akizungumza na wanahabari kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza.

Aidha Dkt. Simbele alisema viashiria vingine vinavyoashiria dalili za ugonjwa wa afya ya akili ni pamoja na watoto kuwa katika hali ya utundu na kutotulia jambo ambalo wazazi na walezi wamekuwa wakishindwa kulibaini mapema wakidhani ni hali ya kawaida kwa watoto.

Alisema wazazi ama walezi wanapooza dalili hizo kwa watoto wao ni vyema wakawawahisha katika matibabu hatua itakayowasaidia kutopata madhara zaidi kutokana na ugonjwa huo wa afya ya akili huku akibainisha kuwa matatizo ya afya ya akili hutokana na lishe duni mama anapokuwa mjamzito 

Katika hatua nyingine Dkt. Simbele aliongeza kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wa afya ya akili wamerithi katika familia zao na kwamba asilimia 50 ya watu wazima wenye ugonjwa huo hutokea wakiwa na chini ya miaka 14.

Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Watoto katika Hospitali ya Kanda Bugando, Dkt. Kiyetia Hauli alisema kwa siku Hospitali hiyo imekuwa ikihudumia wagonjwa kati ya 30 hadi 70 ikiwa ni ishara kwamba tatizo la ugonjwa wa afya ya akili ni kubwa katika jamii.

Kauli mbiu katika Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili 2021 ni "Afya ya Akili Kkatika Ulimwengu usio na Usawa" ikitoa changamoto kwamba huduma za afya ya akili hutolewa katika maeneo ya mijini tu hali ambayo haileti usawa katika utoaji huduma.

No comments:

Powered by Blogger.