LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mahafali Shule ya Balili Bunda, Mkurugenzi KIVULINI awataka wahitimu kujitunza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wasichana na wanawake (KIVULINI), Yassin Ally amewashauri wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka huu kujilinda na kutoruhusu vishawishi hususani vya kimapenzi wakati wakisubiri matokeo nyumbani.

Yassin ametoa rai hiyo Oktoba 13, 2021 wakati akizungumza kwenye mahafali ya 18 ya wahitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Balili B iliyopo Wilaya Bunda mkoani Mara ambapo alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo.

Amesema wajibu wa kwanza wa kujilinda unapaswa kuanza na wahitimu hao wenyewe na siyo wazazi wao na kwamba wanapaswa kujiepusha na vishawishi vya kimapenzi kwani kujiingia kwenye vitendo vya ngono katika umri mdogo kuna madhara makubwa ikiwemo kupata ujauzito.

Naye Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Isaya Mgeta amebainisha kuwa mwaka 2015 wanafunzi 123 waliandikishwa kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo lakini waliohitimu mwaka huu ni wanafunzi 98 wavulana wakiwa ni 50 na wasichana 48 ambapo wanafunzi 25 hawakuhitimu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro.

Naye mmoja wa wahitimu, Asha Tumbu akisoma risala kwenye mahafali hayo amesema shule ya Msingi Balili B inakabiliwa na upungufu wa vyumba 13 vya madarasa kwani vilivyopo ni 10 na mahitaji ni 23 hali inayosababisha mrundikano wa wanafunzi huku pia kukiwa na upungufu wa madawati 87.

Katika mahafali hayo, mgeni rasmi ameanzisha zoezi la kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kudurufu mitihani (photocopy mashine) katika shule hiyo kwa kutoa shilingi laki mbili huku wazazi na waalimu wakitoa shilingi elfu 67 ambapo ametoa rai kwa Kamati ya Maendeleo ya Shule kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu ili kufanikisha zoezi hilo.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI lenye makao makuu jijini Mwanza, Yassin Ally akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba Shule ya Msingi Balili B wilayani Bunda.
Mkuu wa Shule ya Msingi Balili B wilayani Bunda, Mwalimu Isaya Mgeta akizungumza wakati wa mahafali ya wahitimu wa darasa la saba mwaka huu.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akikabidhi vyeti kwa wahitimu wa darasa la saba Shule ya Msingi Balili B wilayani Bunda.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akimbidhi cheti mmoja wa wahitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Balili B.
Wahitimu wa darasa la saba Shule ya Msingi Balili B wilayani Bunda mwaka huu 2021 wakiwa na magamba yao.
Wahitimu wakiingia eneo la tukio.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (wa tano kulia waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na wazazi, waalimu na wahitimu wa darasa la saba Shule ya Msingi Balili B wilayani Bunda.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.