DC Hanang' awaahidi neema wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Akiba
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja akikagua gwaride wakati akifunga mafunzo ya Jeshi la Akiba katika hafla iliyofanyika Viwanja vya Kata ya Nangwa wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja, akihutubia vijana waliohitimu mafunzo hayo.
Na Dotto Mwaibale, Hanang'
Mkuu wa Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara, Janeth Mayanja amefunga mafunzo ya Askari wa Jeshi la Akiba kwa Mwaka 2021 yaliyofanyika Kata ya Nangwa wilayani humo.
Jumla ya wahitimu 83 wamemaliza na kufuzu mafunzo hayo kikamilifu pamoja na mafunzo ya udereva kutoka Chuo cha Nangwa VTC na kukabidhiwa vyeti na Mkuu wa Wilaya hiyo Janeth Mayanja ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Mayanja amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama vilivyowaandaa vijana hao na Wakufunzi kutoka Nangwa VTC kwa Kutoa mafunzo ya udereva bila ya kumsahau Diwani wa Kata na wote waliohusika kwa namna moja au nyingine.
Mayanja amewahakikishia vijana hao kuendelea kuwa mlezi na mshauri wao hususani katika maswala ya ajira na akatoa ahadi ya kuwapa kipaumbele kwenye nafasi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pindi zitakapotoka.
Mayanja ameahidi na kuwapa nafasi za ulinzi kwenye mradi mkubwa wa bomba la mafuta ambalo linapita kwenye vijiji vinne vya wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine Mayanja amewakaribisha SUMA JKT ambao walihudhuria hafla hiyo kwa lengo la kuwasaili vijana hao Ili waweze kuwachukua kwa ajili ya kufanya shughuli za ulinzi na udereva.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, Kamati ya Siasa ya wilaya Ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo Mathew Darema, Mbunge wa Jimbo la Hanang' Mhandisi Samwel Hayyuma ,Mbunge wa Vijana Taifa Asia Halamga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya,wazazi,walezi, wananchi wa Kata ya Nangwa na kata za jirani.
No comments: