LIVE STREAM ADS

Header Ads

Makamu Mkuu CUHAS athibitisha, juisi ya miwa inayouzwa Nyamagana ina kinyesi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mwonekano wa machine inayotumika kuandaa juisi ya miwa / picha kutoka mtandaoni.

Ukuaji wa teknolojia hususani mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na Whatsupp umesaidia upashanaji taarifa kwa haraka miongoni mwa watumiaji wa mitandao hiyo.

Hata hivyo baadhi ya taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa na watumiaji wa mitandao hiyo zimekuwa zikipokelewa kwa hisia tofauti na hata nyingine kuzua taharuki kutokana na kwamba si taarifa zote zinakuwa za kweli.

Hatua hiyo imesababisha maadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kutoamini kwa haraka taarifa wanazokutana nazo kwenye mitandao hiyo hata kama ni za kweli. Hii ni kutokana na taarifa nyingi zinazochapishwa mitandaoni kugubikwa na uzushi mwingi.

Miongoni mwa taarifa iliyochapishwa na mmoja wa watumiaji wa mitandao ya kijamii na kuzua gumzo kwenye majukwaa mbalimbali mitandaoni ni ile iliyoeleza kwamba asilimia kubwa ya juisi ya miwa inayouzwa Nyamagana mkoani Mwanza ina kinyesi.

Taarifa hiyo imechapishwa na mtandaoni na mtu aliyejulikana kwa jina la ‘dr.paulmasua’ ikisomeka “utafiti uliofanywa huko Mwanza na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Bugando unaonyesha kwamba asilimia kubwa ya juice ya miwa inayouzwa Nyamagana ina mavi..!”

Utata mtupu
Muda mfupi baada ya taarifa hicho kuchapishwa mtandaoni ilisambaa kwa kasi na kuzua taharuki na mjadala mzito kwenye majukwaa mbalimbali hususani Whatsupp, kila mmoja akitaka kujua ukweli wake.

Baadhi ya wachangiaji walihoji “kwanza Bugando siyo Chuo Kikuu, ni Hospitali ya Kanda hivyo hii taarifa hatuwezi kuiamini”. Pia kutokana na kutoamini taarifa hiyo, wengine walichapisha maoni yenye mzaha yenye kupotosha kama haya “mavi hayana shida kwenye baridi, nitaendelea kuigida kama kawaida kusafisha figo”.
Chapisho lililozua gumzo mtandaoni.

Ukweli wake ukoje?
Ili kuondoa utata huo, BMG Online Media ilimtafuta Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS- Bugando), Prof. Paschalis Rugarabamu aliyethibitisha kwamba taarifa hiyo ni ya kweli.

“Ni kweli utafiti huo umefanyika na ripoti yake imetolewa kwenye kongamano la kisayansi la 12 lililoandaliwa na CUHAS katika Hoteli ya Malaika. Kesho (Novemba 13) watafiti watakuwa kwenye mahafali hapa Bugando, wataongea na waandishi wa habari ili kuutolea ufafanuzi zaidi” Prof. Rugarabamu ameiambia BMG. SOMA hapa Mtafiti wa juisi za miwa Mwanza

Aidha mmoja wa watafiti kutoka Chuo cha CUHAS ameiambia BMG kwamba kuna aina ya bakteria aitwaye 'Escherichia Coli' anayeishi kwenye takamwili za mfumo wa chakula cha binadamu ama wanyama ambaye akipatikana kwenye chakula, maji au vinywaji mbalimbali huashiria uwepo wa takamwili (kinyesi) kwenye vitu hivyo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS- Bugando), Prof. Paschalis Rugarabamu/ Picha kutoka Maktaba ya BMG.

Ushauri wa bure
Kutokana na ukweli juu ya utafiti huo; watengenezaji, wauzaji na watumiaji wa juisi ya miwa Nyamagana wanashauriwa kuzingatia hatua mbalimbali za usafi kuanzia maandalizi ya kusafisha miwa, maji wanayotumia pamoja na barafu wanayotumia kufanya kinywaji hicho kuwa na ubaridi.

Hatua hiyo itaondoa uwezekano wa kuwa na chembechembe za kinyesi cha binadamu na hivyo kutohatarisha afya kwa watumiaji. Jitihada hizo zisipozingatiwa, watumiaji wa juisi ya miwa inayouzwa Nyamagana na maeneo mengine ya Mwanza wanaweza kuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya kuhara ikiwemo kipindupindu.

Pia mwaka 2019 tahadhari ilitolewa kwa watumiaji wa juisi ya miwa kupitia tovuti ya gazeti la Mwananchi ikiwa na kichwa cha habari ‘Wanywaji juisi ya miwa chukueni tahadahari’ Isome hapa.

Muhimu
Hata hivyo ili kuifanya mitandao ya kijamii kuaminika na kuondoa utata ambao wakati mwingine hujitokeza hata kwenye taarifa ambazo ni sahihi, watumiaji wa mitandao hiyo wanahimizwa kuacha kuchapisha taarifa za uzushi na kujikita kwenye taarifa sahihi.
Na George Binagi-GB Pazzo, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.