LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watu 150 wadakwa kwa tuhuma za mauaji nchini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeunda Kamati ya kuishauri Serikali kuhusu namna ya kufanya katika kupata suluhisho la kudumu katika kuzuia uhalifu na mauaji yaliyokithiri nchini huku ikitoa siku 21 kukamilisha kazi yake na kurudisha mrejesho kwenye wizara hiyo.

Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Hamad Masauni ameyasema hayo Januari 31, 2022 wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma baada ya kikao chake na viongozi wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi ili kutoa mrejesho wa matokeo ya kilichojadiliwa kuhusu kadhia ya matukio ya mauaji yanayoendelea nchini.

Amesema kuundwa kwa Kamati hiyo kutasaidia kupatikana kwa suluhisho la kudumu katika kuzuia mauaji na uhalifu mwingine nchini huku akitaka watanzania kutoa ushirikiano katika kuwabaini wahalifu.

Masauni amesema Kamati hiyo itahusisha jopo la wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka,Takukuru, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Wizara ya Elimu/ Elimu ya Juu.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa kutokana na kukithiri vitendo vya mauaji nchini hadi sasa jeshi la polisi linawashikilia watu 150 kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo huku akitaja mikoa vinara kwa mauaji kuwa ni Kagera, Dodoma, Mara, Songwe na Kigoma.

Ametaja sababu mbalimbali za mauaji hayo kuwa ni pamoja na imani za kishirikina, wivu wa mapenzi, wivu wa maendeleo, visasi, migogoro ya ardhi, mali na ulevi na kueleza kuwa Serikali haiwezi kukaa kimya na kudharau malalamiko ya wananchi.

Hatua hii imekuja zikiwa zimebakia siku mbili tu baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango kutoa siku saba kwa Jeshi la polisi nchini na idara zake zote kutafuta ufumbuzi wa mauaji yanayoendelea nchini.
Na Ditto Kwilasa, Malunde 1 Blog -DODOMA

No comments:

Powered by Blogger.