LIVE STREAM ADS

Header Ads

Sekta ya Madini Tanzania yavutia mataifa mengine Afrika, kuja kujifunza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Tanzania imetajwa kufanya vizuri katika Sekta Ndogo ya Uchimbaji Mdogo wa Madini kutokana na usimamizi madhubuti uliopelekea ukuaji wa shughuli za uchimbaji mdogo hatua ambayo imeifanya nchi ya Zimbabwe kupanga kuwaleta wataalam wake kujifunza zaidi katika eneo hilo.

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo Februari 02, 2022 wakati akizungumza na Vyombo vya Habari baada ya kikao chake na Waziri wa Madini wa Zimbabwe Wiston Chitando, wataalam kutoka nchi hizo pamoja na Sekretarieti ya Umoja wa Nchi zinazozalisha Madini ya Almasi (Association of Diamond Producing Countries – ADPA) na Kimberly Processing Certification System (KPCS) ambayo imeshiriki kwa njia ya mtandao.

Dkt. Biteko alisema nchi hizo zimekutana kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa sekta ya madini pamoja na kujifunza namna bora ya kushirikiana kimaendeleo kwa nchi wazalishaji wa madini ya Almasi Barani Afrika.

Pia aliongeza kuwa kikao hicho kimelenga kuiwezesha nchi ya Zimbabwe kama mwenyekiti mtarajiwa wa umoja huo kujifunza namna ya kusimamia masuala yanayohusu umoja huo pamoja na kupata mrejesho wa namna shughuli zake zinavyoendelea kabla nchi hiyo haijachukua kijiti cha uenyekiti.

Aidha Waziri Biteko alisema Tanzania inayo mengi iliyojifunza kutoka nchi ya Zimbabwe ambayo ni miongoni mwa nchi zilizoanza shughuli za uchimbaji madini kwa muda mrefu ambapo hivi sasa Sekta ya Madini katika nchi hiyo inachangia asilimia 12 katika Pato lake la Taifa ikilinganishwa na Tanzania ambayo hivi sasa mchango wake umefikia asilimia 9.7.

Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado nchi hiyo inakabiliwa na changamoto ya utoroshwaji wa madini hivyo uwepo wake nchini utaiwezesha kujifunza masuala ya udhibiti wa utoroshwaji madini ikiwemo kuwa na Sheria nzuri itakayosaidia kuwepo mabadiliko ya kisekta kama ilivyo kwa Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Madini Zimbabwe Wiston Chitando alisema kuwa haina shaka kuwa Tanzania imekuwa mfano mzuri kwa nchi hiyo kutokana na inavyosimamia Sekta ya madini hususan uchimbaji mdogo wa madini hali ambayo inailazimu nchi hiyo kuwatuma tena watalaam wake kuja nchini kujifunza zaidi ili kuiwezesha nchi hiyo kupiga hatua katika eneo hilo.

Aliongeza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano ya kiuchumi yaliyopo baina ya nchi hizo mbili ikizingatiwa kuwa, nchi hizo zina mambo mengi yanayofanana ikiwemo jiolojia, mifumo wa usimamizi na utoaji leseni za madini na masuala ya kisiasa.

Pia alisema kutokana na nchi hiyo kujiandaa kuchukua uenyekiti wa umoja wa ADPA, imeonelea ipo haja ya kujifunza na kupata uzoefu kutoka Tanzania wa namna ya kusimamia shughuli za umoja huo ili kuboresha mazingira yanayohusu madini ya almasi

Pia alitumia fursa hiyo kuipongeza Tanzania kutokana na kuendelea kusimamia na kuujenga umoja huo.

Katika kikao hicho, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga aliwasilisha taarifa kuhusu Sekta nzima ya madini nchini, mtaalamu kutoka Idara ya Jiolojia, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Ronald Massawe ametoa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini nchini na kuonesha jiolojia ya Tanzania.

Kwa upande wake Meneja wa TEHAMA kutoka Tume ya Madini, Cathbert Simalenga aliwasilisha taarifa kuhusu mfumo wa utoaji leseni za madini na usimamizi wake (Mining Cadastre Management Infomarmation System).

Waziri Chitando na ujumbe wake wanafanya ziara ya siku mbili nchini ambapo pia watapata fursa ya kutembelea masoko mbalimbali ya madini.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Madini

No comments:

Powered by Blogger.