LIVE STREAM ADS

Header Ads

Taasisi ya Aga Khan yatoa mafunzo kwa wanahabari Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Taasisi ya Aga Khan Tanzania (Aga Khan Foundation Tanzania- AKFT) umetoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani Mwanza lengo likiwa ni kuwajengea uwezo kuripoti kwa weledi habari za afya hususani ugonjwa wa Saratani.

Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika Machi 25, 2022 na kuwashirikisha zaidi ya waandishi wa habari 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.

Afisa Mawasiliano kutoka taasisi hiyo, Brendalinny John alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi Mtambuka wa Saratani Tazania (TCCP) unaotekelezwa katika mikoa ya Dare es salaam na Mwanza kwa lengo la kupunguza ugonjwa huo.

Alisema matarajio ya taasisi hiyo ya Aga Khan ni kuona waandishi wa habari wanaripoti habari za afya kwa usahihi hususani zinazohusu ugonjwa wa saratani ili kuisaidia jamii kubadili tabia na mtindo wa maisha hatua itakayosaidia kupunguza viashiria vinavyochochea maambukizi ya saratani.

Meneja Ubia, Uwezeshaji na Mawasiliano kutoka taasisi ya Aga Khan, Dkt. Sarah Maongezi alisema mradi wa TCCP unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mine ukigharimu shilingi bilioni 32 ikiwa ni ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFP) na taasisi ya The Aga Khan Foundation (AFK) huku msaada wa kiufundi ukitolewa na taasisi ya ‘Institute Curie’.

Alisema mradi utasaidia kuboresha miundombinu ya utoaji huduma kwa wagonjwa wa saratani ambapo tayari Hospitali ya Kanda Bugando tayari imepokea mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani ya matiti na kwamba wanatarajia kujenga hospitali ya saratani yenye mashine za kisasa katika Hospitali ya Aga khan Dar es Salaam ili kusaidiana na Hospitali ya Ocean Read Dar es salaam kutoa huduma kwa wananchi.

Akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo kuhusu ugonjwa saratani, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwanza Sekou Toure, Dkt. Athanas Ngambakubi alisema ugonjwa wa saratani unatibika ikiwa mgonjwa atawahi matibabu mapema na hivyo kutoa rahi kwa wanahabari kuelimisha wananchi kutambua umuhimu wa kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo na si kusubiri hadi waone dalili ndipo waende hospitalini.

Alisema kuna aina mbalimbali za saratani ikiwemo saratani ya tezi dume, matiti, ngozi, tumbo, utumbo mpana, ulimi, sehemu ya kutunzia kinyesi, haja kubwa, mapafu, ini, kongosho, figo, ubongo, mbupa, damu na kwamba saratani ni ugonjwa unaosababishwa na kugawanyika kwa seli za kiungo chochote katika mwili wa binadamu bila kufuata utaratibu.

Alisema idadi kubwa ya wanaume huathirika zaidi na saratani ya tezi dume huku wanawake ikiwa ni saratani ya matiti na shingo ya kizazi. Alisema mwaka 2020 kulikuwa na wagonjwa 40,464 wa saratani ambapo kati ya hao zaidi ya elfu 20 walifariki dunia.

Dkt. Ngambakubi alizitaja baadhi ya dalili za saratani kuwa ni pamoja na uvimbe katika sehemu iliyoathirika, mwili kuchoka ikiwa mfumo wa hewa utaathirika, vidonda, majimaji yenye harufu na mwili kupungua uzito na kwamba kwa akina mama hutokwa damu sehemu za ukeni.

Alitoa rai kwa wanahabarikuelimisha wananchi kubadili mtindo wa maisha kama kuacha matumizi ya tumbaku, sihara, ugoro, pombe, ulaji usiozingatia lishe bora na kutofanya mazoezi kwani hizo ni miongoni mwa tabia hatarishi zinazochochea ugonjwa wa saratani.

Aliongeza kuwa kuna baadhi ya wagonjwa hupata saratani kutokana na kupata kemikali mbalimbali hususani maeneo ya kazi pamoja na ngono zembe na kwamba ugonjwa wa kichocho pia una mahusiano ya karibu na saratani ya kibofu cha mkojo na hivyo kuwahimiza wananchi kuwa makini na kemikali mbalimbali kama matumizi ya kemikali shambani kwani huchochea chanzo cha saratani.

Dkt. Ngambakubi alisema baadhi ya saratani pia hutokana na kurithi vina saba kutoka kwa wanafamilia waliowahi kuugua ugonjwa huo, lakini pia umri mkubwa ingawa kuna saratani pia zinawapata watoto wadogo.

Alibainisha kuwa kwa sasa kuna jitihada mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo ikiwemo chanjo kwa saratani ya shingo ya kizazi ambayo ni kinga ya ugonjwa huo, pia homa ya ini ina chanjo na inaweza kusaidia kukinga saratani ya ini.

Dkt. Ngambakudi alitoa rai jamii kubadilisha tabia ikiwemo kuacha ngono zembe na kuzingatia ulaji unaofaa pamoja na kufanya mazoezi kwani ni miongoni mwa tabia zinazosaidia kujikinga na saratani.

Aliwasihi pia kujikinga na kemikali za ina mbalimbali hususani kwa wanaofanya kazi viwandani ama kupulizia dawa mashambani. Alisema ni muhimu pia kwa wananchi kufanya uchunguzi wa mapema na kupata tiba ambayo ni pamoja na upasuaji ama dawa za mionzi wanapobainika kuwa na ugonjwa huo.

Awali akifungua mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Saratani kutoka Hospitali ya Kanda Bugando, Dkt. Beda Likonda alisema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa takwimu zinazohusiana na wagonjwa wa saratani nchini, utoaji elimu kwa wananchi na watoa huduma mbalimbali ili kuepuka viashiria vinavyosababisha ugonjwa huo pamoja na uwekezaji duni kwenye tiba ya saratani na hivyo kuishukuru taasisi ya Aga Khan kwa jitihada zake za kupambana na ugonjwa huo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Richard Makore kutoka gazeti la Nipashe pamoja na Paulina David kutoka RFA walisema yamewaongezea weledi na wataisaidia jamii ili kubadili tabia na kuchukua hatua ya kujikinga na saratani ikiwemo kutambua umuhimu wa kuchunguza ugonjwa huo hata kabla ya kusubiri kuugua.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Afisa Mawasiliano kutoka taasisi Aga Khan Tanzania, Brendalinny John akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Daktari Bingwa wa Saratani kutoka Hospitali ya Kanda Bugando, Dkt. Beda Rikonda akifungua mafunzo hayo.

No comments:

Powered by Blogger.