LIVE STREAM ADS

Header Ads

Hospitali ya Bugando yazindua Mashine ya Kisasa ya Uchunguzi wa Saratani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Hospitali ya Kanda Bugando iliyopo jijini Mwanza imezindua rasmi matumizi ya mashinde ya kisasa (Mammografia) kwa ajili ya uchunguzi wa Saratani ya matiti kwa akina mama ambayo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 800.

Uzinduzi wa matumizi ya mashine hiyo ulifanyika Machi 11, 2022 ukienda pamoja na uzinduzi wa mradi mtambuka wa kupambana na Saratani Tanzania (TCCP), mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliyewakilishwa na Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Kanda Bugando Dkt. Fabian Massaga alisema ugonjwa wa Saratani unatibika ikiwa mgonjwa atawahi matibabu mapema na hivyo kutoa rai kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa ugunjwa mara kwa mara.

Aidha alibainisha kuwa katika kila watu laki moja, kuna wagonjwa wapya 76 wa Saratani huku vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo vikifikia 78 kwa kila vifo 100 ambapo ongezeko hilo linasababishwa na wagonjwa kuchelewa kufika kwenye matibabu.

Naye Meneja Mradi wa TCCP ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tiba kutoka Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan Tanzania, Dkt. Harrison Chuwa alisema mradi huo wa miaka minne unagharimu shilingi bilioni 32 ambapo pamoja na mambo mengine umesaidia Hospitali ya Bugando kupata machine hiyo ya uchunguzi wa Saratani ya matiti ikiwa ni mashine ya tatu nchini.

Dkt. Chuwa alibainisha kuwa zaidi asilimia 50 ya wagonjwa wa Saratani nchini wanaofika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam wanatoka mikoa ya Kanda ya Ziwa hivyo kusimikwa kwa mashine hiyo ambayo ina uwezo wa kuchunguza wagonjwa 20 hadi 25 kwa siku kutapunguza msongamano wa wagonjwa wa Saratani katika Taasisi hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe alisema Saratani ni miongoni mwa magonjwa yanayoathiri maisha ya watu wengi na kwamba uchunguzi uliofanyika mwaka 2021 ulibaini zaidi ya watanzania elfu 40 kuugua ugonjwa huo ambapo aliwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuongeza jitihada za kupamban na ugonjwa huo ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii.

Mradi wa TCCP unafadhiliwa na wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFP) pamoja na taasisi ya The Aga Khan Foundation (AFK) ukilenga kupambana na ugonjwa wa Saratani pamoja na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo katika mikoa ya Dar es salaam na Mwanza.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe (wa pili kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mashine ya uchunguzi wa Saratani ya matiti katika Hospitali ya Bugando.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kanda Bugando, Dkt. Fabian Massaga akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Meneja Mradi wa TCCP, Dkt. Harrison Chuwa akitoa taarifa ya mradi huo.
Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Bugando, Dkt. Fabian Massaga (kushoto) akiwa na wadau wa maendeleo kwenye uzinduzi huo.
Wananchi na wadau mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo.
Mashine mpya na ya kisasa kwa ajili ya uchunguzi wa Saratani ya matiti iliyozinduliwa katika Hospitali ya Kanda Bugando.

No comments:

Powered by Blogger.