LIVE STREAM ADS

Header Ads

RUWASA watakiwa kukamilisha mradi wa maji Mwamagili, Misungwi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umetakiwa kumsimamia ipasavyo mkandarasi ili akamilishe kwa wakati mradi wa maji Mwamagili-Mwagiligili katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel alitoa agizo hilo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya Magu, Salum Kalli kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani yaliyofanyika Machi 22, 2022 wilayani Misungwi.

Alisema mradi huo utakaogharimu shilingi Milioni 826,948,500 kwa awamu ya kwanza unapaswa kukamilika ifikapo Aprili 30, 2022 ili kutoa huduma kwa wananchi na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kusaka maji ambayo hata hivyo si safi na salama.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Robert alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo kwa awamu ya kwanza kiasi cha shilingi milioni 500,620,000 kupitia mgao wa fedha za mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambapo ukikamilika utawanufaisha zaidi ya wananchi elfu 17, mifugo 1,698 na taasisi nne.

Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Misungwi, Frankson Kanyere alisema mradi huo unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ikiwemo bomba za chuma na plastiki na hivyo kusababisha uchimbaji wa mitaro kuchelewa ingawa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji pamoja na vituo vya kuchotea maji unaendelea vyema.

Naye Kaimu Meneja wa RUWASA mkoani Mwanza, Emmanuel Mafuru alisema utekelezaji wa mradi huo ni chachu ya maendeleo kwa wananchi ambapo badala ya kutumia muda mrefu kusaka maji, watajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuwahimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji kama kauli mbiu ya Wiki ya Maji mwaka huu inavyosisitiza ikisema "Maji Chini ya Ardhi, Hazina Isiyoonekana kwa Maendeleo Endelevu".

Baadhi ya wakazi wa Mwamagili wilayani Misungwi akiwemo Majaliwa Lusafija na Lucia Jilala walisema kwa sasa wanakumbana na adha ya kusaka maji kwenye marambo ambayo pia yanatumiwa na mifugo na hivyo kuhimiza mradi huo kukamilika ili kuwaondolea changamoto hiyo.

Mradi wa maji Mwamagili-Mwagiligili ulipaswa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2021/22 lakini haukuanza kwa wakati kutokana na ufinyu wa bajeti umeanza kutekelezwa awamu ya kwanza mwaka huu 2022 kupitia fedha za UVIKO 19 katika Kijiji cha Mwamagili na awamu ya pili utatekelezwa katika Kijiji cha Mwagiligili.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya Magu, Salum Kalli (mwenye koti) akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji boda wa Mwamagili- Mwagiligili Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. Ni baada ya kutembelea ujenzi wa tenki la maji la mradi huo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani. Wengine ni watendaji mbalimbali wa RUWASA.
Mwonekano wa ujenzi wa tenki la maji katika mradi wa Mwamagili-Mwagiligili ambao unasimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Mwonekano wa ujenzi wa vituo vya kuchotea maji katika mradi wa maji Mwamagili-Mwagiligili wilayani Misungwi.
Mkuu wa Wilaya Magu, Salum Kalli akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani 2022 ngazi ya Mkoa Mwanza yaliyofanyika wilayani Misungwi.
Mkuu wa Wilaya Magu, Salum Kalli (kulia) akizungumza kwenye maadhimisho ya Wiki ya Maji wilayani Misungwi.
Kaimu Meneja wa RUWASA Mkoa Mwanza, Emmanuel Mafuru akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Katibu Tawala Wilaya Misungwi Peter Sabatho akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Misungwi, Veronica Kessy (hayuko pichani).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Misungwi, Leokadia Humera akitoa salamu kwenye maadhimisho hayo.
Mwenyekiti Halmashauri ya Misungwi, Machibywa Kashinde akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mwakilishi akina mama akitoa hamasa kwa jamii kutumia maji safi na salama kupitia miradi ya RUWASA hatua itakayowasaidia kuepukana na maradhi mbalimbali ikiwemo kuhara na kichocho.
Watendaji mbalimbali wa RUWASA mkoani Mwanza wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Watendaji wa RUWASA mkoani Mwanza wakifuatilia maadhimisho hayo.
Mshereheshaji akiongoza maadhimisho hayo.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.