LIVE STREAM ADS

Header Ads

Taasisi ya DIT yakabidhi viatu kwa wanafunzi wilayani Ilemela

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) kampasi ya Mwanza imekabidhi jozi 126 za viatu vya ngozi kwa wanafunzi 126 wanaotoka kwenye familia zinazoishi katika mazingira magumu katika Wilaya ya Ilemela mkoani mwanza.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt Albert Mmari amesema viatu hivyo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu vimetengenezwa na wanafunzi pamoja na wajasiriamali wanaopata elimu kwenye taasisi hiyo na vimetolewa ili kuwezesha wanafunzi hao kupata elimu bila kikwazo chochote.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya elimu ikiwemo kujenga madarasa zaidi ya elfu 15 kupitia fedha za UVIKO 19,DIT tumeamua kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa viatu ili kuwezesha kila mtoto kupata elimu kwenye mazingira bora” alisema Dkt. Mmari.

Aidha Dkt. Mmari amesema mkakati wa taasisi ya Teknolojia ya Dar es salam kampasi ya Mwanza ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wanaotoka kwenye familia zisizojiweza kiuchumi.

“Hii ni awamu ya pili ya ugawaji wa viatu kwa wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatutaishia hapa bali tutaendelea kugawa viatu ambapo baada ya kumaliza wilaya ya ilemela,tutaendelea na zoezi hilo katika wilaya zote za mkoa wa mwanza” aliongeza Dkt. Mmari.

Wanafunzi 126 walionufaika na msaada huo wa viatu wanatoka kwenye shule za msingi Sangabuye, Nyafula na Bugogwa ambao wameishukuru taasisi ya DIT kwa kuwawezesha kuondokana na changamoto ya ukosefu wa viatu iliyokuwa inawakabili.

“Naishi na bibi yangu ambaye hana uwezo wa kuninunulia kiatu lakini kwa msaada huu nitakuwa nahudhuria shuleni kila mara make zamani nilikuwa mtoro kwa sababu sikuwa na kiatu” alisema Petro Stephano ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi 26 walionufaika na viatu hivyo katika shule ya msingi Bugogwa.

Kwa upande wa uongozi wa Shule za Msingi Sangabuye, Bugogwa na Nyafula mbali na kuishukuru kwa dhati DIT wamesema msaada huo utasaidia kwa kiasi kukubwa kupunguza tatizo la utoro wa wanafunzi.

“Tuna watoto wengi wenye mahitaji ya viatu, hivyo tunaomba siku nyingine mje na viatu vingi zaidi” alisema Mwita Manoti ambaye ni Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Bugogwa.
Mwonekano wa baadhi ya viatu vilivyotolewa na taasisi ya DIT.
Baadhi ya wanafunzi wakiwa wamevaa viatu vilivyotolewa na taasisi ya DIT.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam Dkt. Albert Mmari (kushoto) akikabidhi kiatu kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sangabuye Patrodi Mpoki (kulia).
Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam Dkt. Albert Mmari (kulia) akikabidhi kiatu kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyafula, Mwl. Evodius Rwiza (kushoto). Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam Dkt. Albert Mmari (kulia) akikabidhi kiatu kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bugogwa, Mwl. Mwita Manoti (kushoto).
Mwonekano wa mwanafunzi miguuni akiwa amevaa viatu vipya vilivyotolewa na taasisi ya DIT na kuvua viatu chakavu alivyokuwa amevaa awali.

No comments:

Powered by Blogger.