LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Gwajima alipongeza Shirika la KIVULINI kwa kuhamasisha wananchi kujenga makazi bora

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Dkt. Dorothy Gwajima (kushoto) wakati huo akiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kabla ya kufanyiwa mabadiliko akizindua nyumba zilizojengwa na wakazi wa Misungwi zilizojengwa kwa hamasa ya Shirika la KIVULINI.
***

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amelipongeza Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI kwa jitihada za kuhamasisha ujenzi wa nyumba bora katika Wilaya Misungwi mkoani Mwanza.

Akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 bungeni jijini Dodoma, Dkt. Gwajima amesema kampeni hiyo ya kuboresha makazi kwa wananchi wenye makazi duni imewezesha kujengwa kwa zaidi nyumba bora 5,000 hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu.
Mwonekano wa moja ya nyumba iliyojengwa katika Wilaya ya Misungwi kutokana na hamasa ya Shirika la KIVULINI.

"Kampeni hiyo ya ujenzi wa nyumba kwa gharama nafuu imekuwa ikifanyika kwa gharama ya kati ya shilingi milioni saba hadi 10 na nyumba inasimama ambapo nyumba hizi zimeongezeka kutoka 751 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 5,002 mwezi Aprili mwaka huu 2022" amesema Waziri Gwajima na kuongeza;

"Tunawashukuru sana Shirika la KIVULINI kwa kutusaidia katika kampeni hii inayowezesha wananchi wenye makazi duni kutumia mifumo ya asili katika kusaidiana kujenga nyumba bora za makazi" ameongeza Waziri Gwajima.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum akiwasilisha bungeni mapendekezo ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2022/23.

Waziri Gwajima pia amepongeza mchango unaotolewa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali likiwemo shirika la KIVULINI katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Shirika la KIVULINI katika kampeni hiyo limekuwa likitumia kauli mbiu ya 'Tupa Nyasi, Weka Bati' kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wilayani Misungwi kuondoa nyumba za nyasi na kujenga nyumba za mabati.

Vikundi 87 vya akinamama vya kusaidiana kujengeana nyumba bora za makazi tayari vimeundwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya Misungwi.
Wanawake wilayani Misungwi wakiwa kwenye moja ya kampeni ya kuhamasisha ujenzi wa nyumba bora za bati na kuachana na nyumba za nyasi.

"Wanachama wa vikundi hivi wanachangiana vifaa vya ujenzi vinavyotumika kujenga nyumba hizi za gharama nafuu, utaratibu huu umewezesha wananchi wengi kupata makazi bora” amesema Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally.

Akizungumzia hatua ya Waziri Gwajima kutambua mchango wa shirika la KIVULINI katika kuboresha makazi, Yassin amesema hatua hiyo imewapa ari ya kuendelea kuhamasisha jamii kujenga makazi bora.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza na wanahabari kuhusiana na kampeni ya ujenzi wa nyumba bora wilayani Misungwi.



No comments:

Powered by Blogger.