LIVE STREAM ADS

Header Ads

Utata ajali ya treni ilitokea mkoani Tabora

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Imeelezwa kuwa chanzo cha ajali ya treni ya abiria iliyotokea Jumatano Juni 22, 2022 mkoani Tabora ni hujuma.

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kuna kipande cha reli kiliondolewa na kisha kurudishiwa kwa kuegeshwa na kusababisha ajali hiyo.

Kadogosa amebainisha kuwa mwendo wa treni hiyo ulikuwa mdogo na kwamba kama ungekuwa wa kasi kubwa basi madhara yangekuwa makubwa zaidi kwa abiria.

"Eneo lililopata ajali treni hiyo lipo jirani na makazi ya watu na mara zote treni za abiria na mizigo huwa zinapita kwa mwendo wa pole" amesema Kadogosa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Honoratha Rutatinisibwa amesema bado wanaendelea na zoezi la kutambua waliofariki na waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo.

Honoratha hakutaka kujibu kama waliofariki ni watatu ama wanne kama taarifa za awali zilivyoeleza ingawa mmoja wa watumishi wa Hospitali ya Kitete ambaye jina lake limehifadhiwa amesema waliofariki ni zaidi ya watu wanane.

Sintofahamu imeibuka baada ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TRC, Jamila Mbarouk kusema waliofariki ni watu wanne na majeruhi 132 huku Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Burian akisema waliofariki ni watu watatu na majeruhi ni 205.
Katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Malolo Manispaa ya Tabora, ilielezwa kuwa watu wanne wanne wamefariki dunia na wengine 132 kujeruhiwa abiria walikuwa wakitoka mkoani Kigoma kupitia mkoani Tabora mpaka Dar es salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Shirika la Reli Tanzania, Jamila Mbarouk alisesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa tano asubuhi ikihusisha treni namba Y.14 yenye injini namba 9019 ikiwa na behewa nane zilizobeba abiria 930 ambapo baada ya kufika eneo la Malolo (Km 10 kutoka Stesheni ya Tabora) behewa tano za abiria daraja la tatu, behewa moja la vifurushi, behewa moja la huduma ya chakula na vinywaji na behewa la breki zilianguka na kusababisha ajali.

Jamila alisema ajali hiyo imesababisha vifo vya watu wanne wakiwemo watoto wawili, wakike mwenye umri wa miaka mitano na wakiume miezi minne na watu wazima wawili, mwanaume na mwanamke pamoja na majeruhi 132 ambapo walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa Kitete - Tabora, kwa ajili ya matibabu na wanaendelea vizuri.
Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza kufanyika uchunguzi na kubaini chanzo chake.

Rais samia ametoa agizo hilo Alhamisi Juni 23, 2022 ambapo pia ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa.

"Nawapa pole wafiwa, nawaombea marehemu wapumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka. Nimeagiza tuliowapa dhamana ya eneo hili kufuatilia na kubaini chanzo na kuchukua hatua stahiki" imeeleza taarifa ya Rais Samia.
BMG Habari kwa msaada wa Mtandao

No comments:

Powered by Blogger.