LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanaharakati wapigwa msasa kuhusu Haki ya Kusema Hapana (Right To Say No)

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wanaharakati 22 kutoka mashirika yanayotetea haki za binadamu Afrika wamekutana Tanzania ili kujengeana uwezo namna ya kuwawezesha wananchi kunufaika na uwekezaji unaofanywa katika maeneo yao.

Mkutano huo wa siku nne tangu Juni 21, 2022 unafanyika jijini Mwanza ukiratibiwa na shirika mwenyeji la HakiMadini lenye makao yake makuu jijini Arusha, linalotekeleza kwa vitendo tamko la kimataifa la Haki ya Kusema Hapana ama Ndiyo (Right To Say No/ Yes) kwa ufadhili wa shirika la WoMin African Alliance la Afrika Kusini.

Katika mjadala wa siku ya kwanza na ya pili, washiriki wamepata fursa ya kujadili Haki ya wananchi Kusema “Ndiyo” au “Hapana” baada ya kuelezwa na wawekezaji faida na hasara za miradi wanayokusudia kuianzisha katika maeneo yao ikiwemo ile ya madini, mafuta na gesi.
Akiongoza majadiliano kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa taasisi ya Africa Transcribe, Evans Rubara alisema wananchi wanayo haki ya kushirikishwa tangu mwanzo katika mchakato wote wa uanzishaji wa miradi inayotokana na rasilimali zinazowazunguka na wao kusema hapana ama ndiyo kabla ya kuachia ardhi yao kupisha miradi hiyo.

“Miradi yote ya kimkakati ikiwemo ya madini bomba la mafuta kutoka Uganda, inachukua mashamba ya wananchi kwa manufaa mapana ya nchi, sasa ni haki wananchi kuelezwa manufaa ya miradi hivyo na namna watafidiwa ili kutoathiri maisha yao baada ya kupisha uwekezaji” alisema Rubara.

Rubara alitahadharisha kuwa Sheria za ardhi ambazo zimekuwa zikitungwa katika mataifa mengi Afrika zimekuwa zikiegemea upande wa mamlaka za Serikali pindi rasilimali chini ya ardhi zinapogundulika hivyo kuna haja pia kufanyia maboresho sheria hizo ili kuwapa nguvu wananchi kunufaika na shughuli za uwekezaji katika maeneo yao.

Kwa upande wake Rose Olokwani ambaye ni Mwakilishi wa wachimbaji wadogo wa madini ya Rubby kutoka Mundarara mkoani Arusha alisema kwa muda mrefu wanawake waliwekwa kando kushiriki kwenye shughuli za madini kutokana na mfumo dume lakini kutokana na jitihada za shirika la HakiMadini kuelimisha wananchi, utamaduni huo umeanza kutoweka na sasa wanawake wameanza kujikita kwenye uchimbaji madini na kujikwamua kiuchumi.

Naye Benadetha Petro ambaye ni mchimbaji madini ya dhahabu katika machimbo ya Mugusu mkoani Geita alisema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa umekutanisha wanaharakati kutoka mashirika mbalimbali ya Afrika na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu namna sekta za uwekezaji zinaendeshwa katika mataifa yao hususani kuwasaidia wanawake kunufaika kiuchumi na raslimali zilizopo katika maeneo yao.
Mkurugenzi wa Shirika la HakiMadini, Zawadi Joseph alisema si kwamba Shirika hilo linapinga wawekezaji bali limekuwa likitoa elimu kwa jamii kuwa na utambuzi wa kukubali masuala yenye tija ama kuwa na haki ya kusema hapana ikiwa uwekezaji huo una madhara kwa jamii.

Alisema changamoto nyingine katika sekta ya madini ni dhana potofu iliyojengeka katika jamii kwamba wanawake hawezi kushiriki kwenye shughuli za uchimbaji madini ambapo amebainisha kuwa Shirika la HakiMadini limekuwa likitoa elimu katika jamii kuondokana na dhana hiyo.

"Katika maeneo ambayo tumefika na kutoa elimu, wanawake wameanza kushiriki kwenye uchimbaji madini na wamewaajri wanaume kwenye migodi yao" alifokeza Zawadi.
Washiriki wa mkutano huo wanatoka mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Afrika Kusaini, Zimbabwe na Cameroon.
Mkurugenzi wa taasisi ya Africa Transcribe, Evans Rubara (kulia) akiongoza majadiliano kwenye mkutano huo uliojumuisha wawakilishi wa mashirika yanayotoka katika mataifa ya Afrika yenye raslimali mbalimbali ikiwemo madini, mafuta na gesi.
Mwakilishi kutoka shirika la WoMin African Alliance nchini Cameroon, Georgine Kengne (kulia) akizungumza kwenye mkutano huo. Kengne alitahadharisha kuwa baadhi ya miradi imekuwa na madhara kwa wananchi ikiwemo uharibifu wa mazingira hivyo ni vyema wananchi kushirikishwa na kutoa maamuzi hatua itakayosaidia kujiepusha na madhara hayo.
Washiriki wakifuatilia mkutano huo.
Mkutano huo uliwashirikisha wachimbaji wadogo wa madini/ wanawake ambao walijengewa uwezo na shirika la HakiMadini na sasa wananufaika kiuchumi na shughuli za uchimbaji madini.
Washiriki kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbambwe, Afrika Kusini na Cameroon wakifuatilia mkutano huo ulioratibiwa na shirika la HakiMadini kwa ushirikiano wa karibu na taasisi ya AfricaTranscribe kwa ufadhili wa shirika la WoMin African Alliance.
Mkutano huo utatoka na mikakati pamoja na maazimio ya pamoja yatakayochochea mabadiliko ya sera na sheria katika mataifa mbalimbali Afrika ili kutoa fursa kwa wananchi kujumuishwa kwenye uchumi wa raslimali mbalimbali ikiwemo madini, mafuta na gesi.
Tazama BMG TV hapa chini
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

No comments:

Powered by Blogger.