LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la EMEDO latahadharisha uchafunzi wa Ziwa Victoria

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Sehemu ya mwonekano wa Ziwa Victoria jijini Mwanza.
***

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo (EMEDO) limetahadharisha kuwa shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika fukwe za ziwa Victoria, zinatishia ghuba ya Ziwa hilo iliyopo Luchelele jijini Mwanza na kwamba ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa mapema kuna hatari ya ikatoweka.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Edtrudith Lukanga ametoa tahadhari hiyo Juni 02, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika ofisini kwake ikiwa ni mwendelezo wa kukutana na wadau mbalimbali kabla ya kuelekea kwenye hafla ya usiku wa wanahabari na wadau Kanda ya Ziwa unaotarajiwa kufanyika Juni 03, 2022 jijini Mwanza.

Lukanga amesema shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo katika ghuba hiyo ambayo husaidia Ziwa kupumua ni hatari kwani zinasababisha kemikali za kilimo na udongo kuingia ziwani na kutishia kutoweka huku zikisababisha pia madhara kwa viumbe hai ikiwemo samaki.

Amesema Ziwa Victoria ni raslimali kubwa inayopaswa kulindwa na kila mmoja ambapo kwa upande wa shirika la EMEDO limekuwa likielimisha jamii katika utunzaji wa Ziwa hilo hususani kutotupa ovyo taka za plastiki.

“Tuna kampeni ya kuhamasisha kila mmoja awajibike katika utunzaji wa mazingira ambapo katika mitaa 10 ya Kata ya Luchelele tumeanzisha vikundi vinavyopita kaya kwa kaya kutoa elimu na pia kukusanya taka na kuzipeleka katika vituo maalum. Tunawahimiza kuona taka kama rasilimali ambapo wenye mawazo ya ubunifu tunawawezesha na kutengena bidhaa mbalimbali” amesema Lukanga.

Pia Lukanga ameongeza kuwa shirika hilo kupitia mwongozi wa kuendeleza uvuvi mdogo ili kuhakikisha unakuwa endelevu kwa mstakabali wa chakula na kujikwamua kiuchumi huku pia wakiwasaidia wavuvi kuondokana na changamoto za kiusalama ziwani.

Naye mmoja wa waandishi wa habari jijini Mwanza, Alphonce Tonny amesema wako tayari kushirikiana kwa karibu na shirika la EMEDO ili kuielimisha jamii kutambua umuhimu wa kutunza mazingira hususani Ziwa Victoria ili kuendelea kuilinda raslimali hiyo muhimu nchini na duniani kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Shirika la EMEDO, Edtrudith Lukanga akizungumza na wanahabari walipotembelea ofisini kwake.
Mkurugenzi wa shirika la EMEDO, Edtrudith Lukanga akizungumza na timu ya wanahabari waliomtembelea ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya kukutana na wadau mbalimbali kabla ya kilele cha hafla ya Usiku wa Wanahabari Kanda ya Ziwa.
Ugeni kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC) ikiwa katika ofisi za EMEDO.
Mkurugenzi wa Shirika la EMEDO, Edtrudith Lukanga (kushoto) akielezea kazi za ubunifu zinazofanywa na vijana waliojengewa uwezo na shirika hilo na hivyo kusaidia kupambana na taka za plastiki kwa kuzitumia kama malighafi.
Mwonekano wa Kituo cha Taarifa na Maarifa ya Mazingira kilichojengwa katika ofisi za EMEDO kwa kutumia taka za plastiki zaidi ya elfu tatu na hivyo kusaidia kupambana na uchafuzi wa mazingira kwani taka hizo kama zisingetumika kwenye ujenzi huo, huenda zingekuwa chanzo cha uchafunzi Ziwa Victoria.
Picha ya pamoja wanahabari na viongozi wa EMEDO.

No comments:

Powered by Blogger.