LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wadau waomba vifaa vya uokoaji majini kushuka bei

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mratibu wa mradi wa kupunguza ajali za kuzama majini Arthur Mugema wakati akiongea na waandishi wa habari.
***

Na Tonny Alphonce, Mwanza
Serikali imeombwa kuondoa ushuru kwa bidhaa za uokoaji majini ili kutoa nafasi kwa wavuvi na wasafiri wa majini kununua bidhaa hizo kwa bei ya kawaida.

Ushauri huo ulitolewa Juni 02, 2022 na Mratibu wa mradi wa kupunguza ajali za kuzama majini kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo Tanzania (EMEDO), Arthur Mugema wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.

Arthur alisema kutokana na vifaa vya kuzuia kuzama watu majini zikiwemo Jaketi maalumu kuwa bei ghali wavuvi wengi hukimbilia kununua Jaketi za bei nafuu ambapo ajali ikitokea Mvuvi anaweza kuzama na kufa maji kutokana na Jaketi aliyonayo kutokuwa na ubora unaotakiwa.

Alisema kutokana na kipato cha wavuvi kutokuwa kikubwa ni vema Serikali ikaangalia uwezekano wa kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vyote vya usalama vinavyotumika majini ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaofanya shughuli zao za kiuchumi majini.
Arthur alisema Jaketi la kujiokolea majibu lenye ubora na usalama linauzwa kuanzia shilingi 40,000 hadi 50,000 kiasi ambacho ni kikubwa kiasi kwamba Wavuvi wadogo hawawezi kumudu gharama hiyo.

“Ukiachilia mbali Imani za kishirikina za kukataa kuvaa majaketi ya kuwazuia kuzama lakini na bei nayo ni kikwazo kikubwa hivyo wavuvi wengi huamua kutovaa na matokeo yake ajali inapotokea wengi wao hufariki dunia” alisema Arthur.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa EMEDO, Editrudith Lukanga alisema katika kuhakikisha jitihada zinachukuliwa za kupunguza vifo vya majini tayari shirika la EMEDO kwa kushirikiana na Taasisi kutoka Wingereza inayohusika na masuala ya usalama kwenye maji na uokoaji RNLI wameingia mkataba wa miaka mitatu wa kusaidia jamii za wavuvi.
Mkurugenzi Mtendaji wa EMEDO Editrudith Lukanga.


“Eneo hili la ajali za majini limesahaulika kiukweli mara nyingi tumekuwa tukisikia au kuona elimu ya usalama barabarani inatolewa au takwimu za ajali za barabarani zikitolewa lakini ajali za majini huoni jitihada kubwa zikichukuliwa kuhakikisha ajali hizo hazitokei” alisema Lukanga.

Alisema Mradi huu ni wa kwanza kutekelezwa Ziwa Victoria na Unagharimu shilingi Bilioni 2.7 na unatekelekelezwa kwa miaka mitatu ukilenga kupunguza hatari za kuzama majini kwa jamii ya wavuvi waliko mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.

“Tayari tumeanza kutekeleza mradi huu na vijana wetu tayari wapo kazini ambapo wengine wapo mkoani Kagera kwa sasa na tunaendelea kutekeleza mradi huu tukishirikiana na serikali” alisema Lukanga.

Wavuvi 231 kati ya 100,000 wanaofanya shughuli zao na kuishi pembezoni mwa Ziwa Victoria wanapoteza maisha kwa mwaka kwa kuzama majini.

Shirika la EMEDO ni miongoni mwa wadhamini wa Usiku wa Waandishi wa Habari na Wadau wa Habari Kanda ya Ziwa ulioandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) utakaofanyika tarehe 03/06/2022 katika ukumbi wa Rock City Mall Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.