LIVE STREAM ADS

Header Ads

Maafisa Utumishi wahimizwa kujiunga na HROAT

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewahimiza watumishi mkoani humo kujiunga na Chama cha Maafisa Utumishi na Utawala Tanzania (HROAT) ili kunufaika na fursa mbalimbali za kiutumishi kupitia chama hicho.

Mhandisi Gabriel ametoa rai hiyo Juni 11, 2022 wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusiana na Mkutano Mkuu wa pili wa HROAT unaotarajiwa kufanyika Juni 15-17, 2022 jijini Mwanza.

Amesema chama hicho kilichoanzishwa mwaka 2018 kimelenga kuwaunganisha maafisa utumishi/ rasilimaliwatu na utawala ili kubadilishana uzoefu na kuishauri pia Serikali namna bora ya usimamizi wa watumishi wa umma na sekta binafsi kuhusu utendaji unazingatia weledi na wenye tija.

Amewakumbusha maafisa watumishi/ rasilimaliwatu na utawala zaidi ya 400 watakaohudhuria mkutano huo kutumia fursa hiyo kutembelea vivutuo mbalimbali vya utalii vilivyopo jijini Mwanza ikiwemo Kisiwa cha Saanane ili kujifunza fursa mbalimbali zilizopo jijini Mwanza.

Naye Mjumbe wa Kamati Tendaji ya maandalizi ya mkutano huo, Monica Andrew amesema umoja huo unajumuisha maafisa rasilimaliwatu na utawala kutoka Serikali za Mitaa, Serikali Kuu pamoja na Sekta Binafsi.

Amesema umoja huo ni injini ya uendeshaji wa taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi na kwamba unairahisishia pia Serikali kufanya idara ya utumishi kuwa rahisi pamoja na kuhamisha Haki na Wajibu baina ya mwajiri na mwajiriwa.

Mkutano huo utaambatana na kaulimbiu isemayo 'Uwepo wa Takwimu za Uhakika, ni Msingi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Twendeni Tukahesabiwe kwenye Sensa ya mwaka 2022'.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Maafisa Utumishi na Utawala Tanzania (HROAT) kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa pili wa chama hicho.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Maafisa Utumishi na Utawala Tanzania (HROAT) kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa pili wa chama hicho.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Maafisa Utumishi na Utawala Tanzania (HROAT) akizungumza na wanahabari kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa Pili wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika jijini Mwanza.
Wanahabari wakiwajibika.

No comments:

Powered by Blogger.