LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la 'Mikono Yetu' lakabidhi vyerehani kwa wasichana waliohitimu mafunzo ya ushonaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Mikono Yetu limekabidhi vyerehani tisa kwa wasichana kutoka Kata ya Buswelu Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza ili kuwawezesha kujikwamu kiuchumi baada ya kuhitimu mafunzo ya ushonaji nguo za aina mbalimbali.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Msichana ni Tai unaotekelezwa na shirika hilo kwa lengo la kuwajengea uwezo na ujuzi wasichana walio nje ya shule ili kuwasaidia kufikia malengo na ndoto zao.

Akizungumza Juni Mosi 2022 wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyerehani hivyo iliyofanyika katika ofisi za shirika hilo zilizopo Buswelu, Msimamizi Mkuu wa mradi wa Msichana ni Tai, Halima Juma amesema wasichana 300 kutoka Mitaa ya Kata ya Buswelu wamejengewa uwezo kujitambua pamoja na ujuzi wa aina mbalimbali tangu mradi uanze mwaka 2020.

Amesema shirika la Mikono Yetu limekuwa likitumia kitabu chake chenye simulizi za Malkia waliotawala nchini kuanzia karine ya 16 hadi 18 ili kuwajengea uwezo wasichana kujiamini, kuwapa ujuzi wa aina mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, elimu ya afya ya uzazi pamoja na kutambua haki na wajibu wao katika jamii.

“Baada ya kuwapa elimu ya kujitambua tulisikiza ndoto zao ambapo wapo waliotaka kuwa mafundi cherehani, wanahabari, madereva wa magari na pikipiki pamoja na urembo ambapo tuliwatenga kupitia makundi yao na kuwatafutia mafunzo ili kutimiza ndoto zao” amesema Halima.

Halima amebainisha kuwa wasichana waliochagua ushonaji wa nguo walipata mafunzo kupitia vituo vilivyofunguliwa na shirika la Mikono Yetu katika Kata ya Buswelu na baadae wasichana tisa walipata ufadhili wa kuongeza ujuzi katika Chuo cha Mafunzo Bugisi mkoani Shinyanga na baada ya kuhitimu, shirika limewakabidhi vyerehani hivyo, lengo likiwa ni kuwa waalimu kwa wenzao lakini pia kuanza uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi.

Nao baadhi ya wasichana waliohitimu mafunzo hayo ambao ni Agnes Juma pamoja na Neema Audax wamesema Shirika la Mikono Yetu limebadili fikra zao na kuwasaidia kutimiza ndoto zao huku wakiwawezesha wenzao kupata ujuzi walioupata.

Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Kata ya Buswelu, Winfrida Gyunda aliyemwakilisha Diwani wa Kata hiyo amelipongeza shirika la Mikono Yetu kwa kazi kubwa ya kubadili maisha ya wanajamii na kwamba wasichana waliopata mafunzo hayo watakuwa mabalozi na waalimu kwa wenzao ambapo amewahimiza kupitia vikundi vyao kuomba mikopo inayotolewa na Halmashauri ili kuimarisha shughuli zao.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Buswelu, Winfrida Gyunda akiongea na wasichana waliopata mafunzo ya ushonaji kupitia Shirika la Mikono Yetu kabla ya kuwakabidhi vyereheni vilivyotolewa na Shirika hilo. Kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Mikono Yetu, Maimuna Kanyamala.
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Buswelu, Winfrida Gyunda akiongea na wasichana waliopata mafunzo ya ushonaji kupitia Shirika la Mikono Yetu kabla ya kuwakabidhi vyereheni vilivyotolewa na Shirika hilo.
Diwani wa Viti Maalum Kata ya Buswelu, Winfrida Gyunda akishuhudia nguo zilizoshonwa na wasichana waliopata mafunzo ya ushonaji kupitia Shirika la Mikono Yetu.
Wafanyakazi wa shirika la Mikono Yetu wakiwa kwenye picha ya pamoja na wasichana waliohitimu mafunzo ya ushonaji katika Chuo cha Bugisi wakati wa hafla ya kuwakabidhi vyerehani ili vitakavyowasaidia kuanzisha mradi wa ushonaji na kuwafundisha pia wenzao.
Wazazi wakiwa na wasichana waliohitimu mafunzo ya ushonaji nguo kupitia shirika la Mikono Yetu.
Viongozi na Watendaji wa Serikali Kata ya Busweli wilayani Ilemela wakiwa kwenye picha ya pamoja na wasichana waliohitimu mafunzo ya ushonaji nguo ambao wamekabidhiwa vyerehani na shirika la Mikono Yetu.
Baadhi ya wasichana waliohitimu mafunzo ya ushonaji nguo mwezi uliopita katika Chuo cha Bugisi mkoani Shinyanga wakiwa kwenye vyerehani walivyokabidhiwa na Shirika la Mikono Yetu lililopo Buswelu wilayani Ilemela.

No comments:

Powered by Blogger.