LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mkandarasi atakiwa kukamilisha mradi wa maji Butimba, Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemtaka mkandarasi kampuni ya SOGEA SATOM na mwenzake VINCI GRAND wote kutoka Ufaransa, kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati mradi wa maji Butimba jijini Mwanza ili kuondoa adha iliyopo.

Waziri Aweso ameyasema hayo Ijumaa Julai 22, 2022 alipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi huo ambao ujenzi wake ulianza Februari 2021 ukitarajiwa kukamilika Februari 2023 kwa gharama ya shilingi bilioni 69.

Amesema Mkandarasi anayetekeleza mradi huo hana changamoto yoyote ikiwemo ya kifedha hivyo anapaswa kuongeza nguvu kazi na kuukamilisha na kwamba Wizara haitakuwa tayari kuona ukitekelezwa kinyume na mkataba.

Naye Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa chanzo kipya cha maji kutoka Ziwa Victoria pamoja na kituo cha kutibu maji chenye uwezo wa kuzalisha majisafi na salama lita milioni 48 kwa siku.

Utekelezaji wa mradi wa maji Butimba umefikia asilimia 35 na baada ya kukamilika utahudumia wakazi zaidi ya laki nne walio maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Mwanza ikiwemo Usagara, Kisesa, Buhongwa Mashariki, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri, Igoma na Buswelu.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.