LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi watakiwa kuwa na mahusiano mazuri na wawekezaji

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amezitaka jamii zinazonguka maeneo ya migodi kutangaza mazuri yanayofanywa na wawekezaji katika Sekta ya Madini ili kuwatia moyo wa kufanya shughuli za madini.

Dkt. Biteko aliyabainisha hayo Julai 22, 2022 akiwa katika ziara yake kijiji cha Kagerankanda wilaya ya Kasulu alipotembelea mgodi wa Kampuni ya Life Business unaochimba madini ya Chokaa mkoani Kigoma.

Alisema migogoro baina ya wawekezaji katika Sekta ya Madini na wananchi katika maeneo mengi ya migodi imewafanya wawekezaji kupata hofu ya kuwekeza katika uchimbaji wa madini katika baadhi ya maeneo na hivyo kupunguza uzalishaji.

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanajenga mahusiano mazuri na wawekezaji ili kutatua changamoto zinazojitokeza kati yao ili wawekezaji waweze kutekeleza huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi.
Aidha Dkt. Biteko aliahidi kuwa changamoto zilizopo za ukosefu wa barabara na ujenzi wa madarasa zitafanyiwa kazi haraka baada ya kutoa maelekezo kwa mwekezaji huyo.

Kwa upande wake mmiliki wa mgodi huo, Lister Balegele ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) alisema kampuni hiyo imekuwa ikilipa mapato ya Serikali na michango mbalimbali kutokana na mauzo ya madini ya chokaa.

Kuhusu huduma za kijamii, Balegele alisema mgodi unajenga madarasa mawili mpaka sasa katika shule ya sekondari hapo kijijini, wametoa madawati 50 kwa ajili ya shule pamoja na kugawa kompyuta mpya kwa shule ya sekondari na msingi.

Baada ya ziara hiyo, mwekezaji wa mgodi huo aliahidi kukamilisha barabara na ujenzi wa madarasa hivi karibuni.

Naye Mjiolojia Mwandamizi kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), John Kalimenze alisema Serikali kupitia taasisi hiyo itaendelea kufanya tafiti za madini ili iweze kugundua maeneo zaidi kwa ajili ya uchimbaji na kuongeza tija kwa wachimbaji na kuongeza mapato ya Serikali.

Aidha alimuhakikishia mwekezaji kupata ushirikiano wa kitaalamu toka GST katika kuendeleza mgodi wake kwa kutambua ubora na wingi wa mashapo ya malighafi ya mawe ya chokaa yaliyopo katika leseni au eneo lake.

Mgodi huo kwa sasa unachimba madini ya chokaa na kusafirisha yakiwa ghafi na kuuza katika kiwanda cha Burundi Cement Company (BUCECO) kupitia mpaka wa Manyovu.
Na Steven Nyamiti, WM

No comments:

Powered by Blogger.