LIVE STREAM ADS

Header Ads

DODOMA: Benki ya CRDB yakabidhi madarasa wilayani Kongwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Benki ya CRDB kanda ya kati Dodoma, imeikabidhi Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma vyumba viwili vya madarasa na madawati 100 kwa shule ya Sekondari Chitego ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha elimu.

Akipokea vyumba hivyo na madawati hayo ambapo kwa jumla vimegharimu shilingi milioni 40, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Mwema ameipongeza na kuishukuru CRDB kwa mchango huo ambao unalenga kukuza na kuboresha elimu.

"Kwa dhati kabisa naishukuru Menejimenti nzima ya Benki ya CRDB kupitia, Meneja wa Kanda ya Kati Ndugu Chabu Mishwaro, Meneja Tawi la Gairo Ndugu Victoria Nyigo kwa kutupa heshima hii ya kipekee kupitia mchango huu uliotolewa na Benki ya CRDB ambao una lenga katika kukuza na kuboresha viwango vya elimu katika wilaya yetu ya Kongwa" alisema Mwema.
Aidha Mkuu wa wilaya alisema kuwa Nchi nyingi zilizoendelea duniani zimepata mafanikio kutokana na kuwekeza katika elimu na Kwa kulitambua hili Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitilia mkazo katika kuboresha mazingira ya elimu nchini.

Aliongeza kuwa kupatikana kwa vyumba hivyo vya madarasa ni hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto iliyopo ya uhaba wa madarasa pamoja na kuboresha miundombinu ya utoaji elimu.

"Niseme tu kwamba Kwa kiasi kikubwa vyumba hivi vya madarasa pamoja na madawati haya yatasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati ya kukalia ambayo yamekuwa yakiikumba shule hii kwa muda mrefu sasa hivyo Benki ya CRDB mmesaidia kuboresha mazingira ya kusomea na kufundishia kwa wanafunzi na walimu wa shule hii" aliongeza.
Alisema Hatua hiyo inasaidia kufikia lengo la kuwapa watoto haki yao ya msingi ya kupata elimu, kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu(SDG) 2030.

DC Mwema alitoa wito kwa CRDB kuzidi kushirikiana na Serikali na jamii kwa ujumla katika kutatua changamoto mbalimbali, ili kwa pamoja waweze kuliletea taifa maendeleo huku akiahidi nao bega kwa bega huku akitoa wito kwa jamii inayozunguka shule hiyo kuitunza.

"Leo hii Benki ya CRDB wanatukabidhi madarasa haya mawili yaliyo jengwa kwenye kiwango cha hali ya juu pamoja na na madawati 100, ni jukumu letu kuhakikisha tunayatunza vizuri ili yaweze kutumika kwa muda mrefu na kuwanufaisha watoto wengi Zaidi" alisema Mwema
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya kati wa Benki ya CRDB, Chabu Mishwaro aliupongeza oongozi mzima wa Halmashauri ya Kongwa kwa mipango mbalimbali ya maendeleo inayobuniwa kila siku na kuisimamia inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania katika Nyanja mbalimbali.

"Ni jambo la wazi kuwa mnafanya kazi kwa bidii, umakini na weledi mkubwa ili kuchangia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto mbalimbali zinazoakabili wananchi wa Kongwa" alisema.

Aliongeza kuwa utendaji kazi wa Viongozi wa Wilaya ya Kongwa umekuwa wa kuigwa na ndio maana wadau mbali mbali wa maendeleo wakiwemo na wao wamehamasika kuungana nao katika kutatua changamoto hizo.
Aliongeza kuwa Benki ya CRDB ni muumini mkubwa sana wa falsafa ya kusaidia jamii ili kuondokana na changamoto mbalimbali ambazo zinarudisha maendeleo na juhudi kubwa za maendeleo nyuma hivyo dhamira hiyo imepelekea banki yao kujiwekea sera maalumu ya kusaidia jamii inayojulikana kama CRDB BANK COOPERATE SOCIAL INVESTMENT POLICY.

"Sera hii inaagiza na kuelekeza Benki yetu kutenga asilimia moja ya faida kila mwaka ili ziende katika shughuli ya kusaidia jamii hususani katika Nyanja ya elimu, afya , mazingira na uwezeshaji kwa ujasiliamali hasa wanawake na vijana" aliongeza.

Alisema Benki ya CRDB inatambua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya elimu ikiwemo ukosefu wa madarasa ya kutosha kuweza kukidhi idadi ya wanafunzi, uhaba wa madawati, upungufu wa matundu ya vyoo, na tunatambua ili Taifa letu liweze kusonga mbele ni lazima tuwekeze katika kuboresha sera na miundombinu ya elimu.
"Ndugu mgeni Rasmi tulivyopokea maombi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuhusu kusaidia kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa na madawati hususani katika shule ya sekondari ya Chitego, ukweli tuliguswa sana" alisema Mishwaro.

Naye Diwani wa Kongwa, Peter Kalunju aliishukuru na kuipongeza Benki ya CRDB kwa msaada huo wa ujenzi wa madarasa na madawati kwani utapunguza changamoto iliyokuwa inaikabili kata hiyo na anaamini majengo hayo yatakuwa chachu ya ufaulu kwa kiwango kikubwa.
Shule ya Chitego Sekondari ni shule mpya ambayo imeanza kutumika rasmi mwaka huu 2022, Shule hii imefanikiwa kusajili wanafunzi 94 kwa idadi ikiwa ni kidato cha kwanza tu kwa mwaka huu, Shule hii ilianza kujengwa kupitia nguvu za wananchi waliojitoa kwa hali na mali ambapo walifanikiwa kujenga madarasa 4 ambayo bado hayajakamilika.
Na Maganga Gwensaga Dodoma

No comments:

Powered by Blogger.