LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kiwanda cha Shaba kuanzishwa mkoani Ruvuma

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Kiwanda cha kuchenjua Madini ya Shaba kinatarajiwa kuanzishwa katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ili kuwezesha shughuli za kuchenjua madini hayo kufanyika nchini na hivyo kulinufaisha taifa na watanzania.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko Agosti 16, 2022 akiwa jijini Mwanza alipokutana na viongozi wa kampuni ya Mineral Access System Tanzania inayotarajia kujenga kiwanda cha kuchenjua madini ya Shaba katika eneo la Mbesa wilayani Tunduru.

Dkt. Biteko aliwapongeza kuwekeza nchini kwani uwepo wake utasaidia kuongeza thamani ya madini na hivyo kuongeza tija ya kiuchumi kwa taifa na kwa wanachi wa Tunduru.

Alisema Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji ili kuwekeza katika Sekta ya Madini kwa kuwa tayari imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwenye mnyororo wote wa shughuli za madini ikiwemo shughuli za utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani madini nchini bila changamoto yoyote.

"Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza katika Sekta ya Madini ili Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo" alisema Dkt. Biteko.

Vile vile Dkt. Biteko alisema Serikali itahakikisha inaweka mazingira wezeshi ili kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa mizigo kuingia nchini kutokana na taratibu za forodha. Aidha alisisitiza kuwasilisha changamoto hiyo katika mamlaka husika.

Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Metallica Commodities Corp, Glendon Archer alisema kiwanda hicho kitawezesha kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo hayo na kuongeza Pato la taifa.

Pia aliahidi kushirikiana na Serikali katika kipindi chote cha uzalishaji ili manufaa ya kiwanda hicho yabaki nchini.

Archer alimshukuru Dkt. Biteko kwa ushirikiano anaopatiwa na Wizara ya Madini katika kila hatua ili kuweza kujenga kiwanda hicho na kuanza uzalishaji.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Daimu Mpakate alisema kiwanda hicho kitaongeza fursa mbalimbali kwa wananchi na Serikali.

Aliongeza kuwa wawekezaji hao wa madini ya Shaba watatoa ajira na kuboresha miundombinu ya maeneo hayo hususan kwa wakazi wa Tunduru.

Kampuni ya Mineral Access System Tanzania pia inatarajiwa kuwekeza kwenye madini ya Lithium na Nikeli nchini.
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko.
Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Metallica Commodities Corp, Glendon Archer.
Na Steven Nyamiti, WM

No comments:

Powered by Blogger.