LIVE STREAM ADS

Header Ads

TCB yatumia Maonesho ya Nanenane Mwanza kuelimisha wakulima

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) inaendelea na utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo Bora na cha kisasa ambacho kitaleta tija na kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao hilo na kuongeza kipato kwa wakulima hali itakayosaidia kuondokana na umasikini.

Akizungumza kwenye Maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) Kanda ya Ziwa Magharibu yanayofanyika Nyamhongolo jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi TCB, James Shimbe amesema elimu hiyo ni endelevu na hivi sasa wanawaelimisha wakulima nchi nzima ili waweze kujikita kwenye kilimo Cha pamba kinachozingatia Kanuni bora. 

Amesema pamoja na kutoa elimu kwa wakulima, pia wana jukumu la kusimamia zao la pamba kuanzia kwenye kuzalisha kwa wakulima, kuvuna, kusafirisha kwenda kwenye soko na kuchakata kwenye viwanda hadi kuuza ndani na nje ya nchi.

"Sisi tupo kwa ajili ya kuwaonyesha wakulima namna pamba inavyozalishwa kuanzia mwanzo hadi kufikia kupata nyuzi na hadi hatua ya mwisho ya mlaji ambapo anapata mafuta ya kula, nguo pamoja na zao lenyewe kama mnyororo wa thamani" amesema Shimbe.

Ameeleza kuwa uzalishaji wa pamba umekuwa ukipanda na kushuka kulingana na mabadiliko ya tabianchi, mvua inapokuwa kubwa inaathiri uzalishaji huku ukame pia ukichochea kuharibu kutokana na zao lenyewe kutokuwa na mfumo wa kufanya umwagiliaji.
Ameongeza kuwa wamekuwa wakisisitiza sana elimu hasa kwenye uzalishaji wa pamba kwa kutumia vigezo sahihi ikiwemo kunyunyiza viuadudu kwenye mashamba.

"Kuna changamoto mbalimbali kwenye zao la pamba ikiwemo wadudu waharibifu waitwao Chawajani, lakini tumejitahidi kuwadhibiti kwa kushirikiana na watafiti kutoka Chuo cha Kilimo Ukiriguru kwa kusambaza viuadudu zaidi ya milioni tisa kwa msimu uliopita 2021/22 ili kukabiliana na wadudu hao wanaochagizwa na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumzia hali ya uzalishaji, Shimbe amesema msimu uliopita walizalisha tani 148,000 ambapo uzalishaji huo uliongezeka ikilingamishwa na msimu wa mwaka 2020/21 ambapo kulikuwa na tani 122,000 na kwamba ongezeko hilo lilitokana na elimu ambayo wanaitoa kwa wakulima.

Ameongeza kuwa hapo awali kulikuwa na utaratibu wa kupanda miche 22,222 kwenye hekari moja lakini kwa sasa wakulima wanashauriwa kupanda miche 44,444 kwa kufuata mstari hatua inayoongeza uzalishaji zaidi.

Shimbe ametoa shukurani kwa wakulima kwa namna ambavyo wanaitumia elimu wanayopewa kwani imesaidia kuleta mabadiliko na utofauti mkubwa kiuzalishaji ikilingamishwa na hapo misimu iliyopita.

Lengo la TCB ni kuwafikia wakulima wengi zaidi ambao wako kwenye mikoa zaidi ya 17 nchini ili kuwaelimisha kujikita kwenye kilimo cha pamba chenye tija.
Mkurungenzi wa Huduma za Usimamizi, TCB, James Shimbe akiwa kwenye Maonesho ya Nanenane jijini Mwanza.
Asilimia 60 ya madaraja ya Pamba nyuzi husafirishwa nje ya nchi na asilimia 40 hubaki nchini kwa shughuli mbalimbali ikiwemo za viwandani.
Mwonekano wa Pamba nyuzi katika Banda la TCB lililopo kwenye Maonesho ya Nanenane Nyamhongolo jijini Mwanza.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.