LIVE STREAM ADS

Header Ads

TBS Mwanza yateketeza shehena ya bidhaa zilizoisha muda, zenye viambata sumu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
 Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefanikiwa kukamata na kuteketeza shehena ya vipodozi na chakula zaidi ya tani tatu zenye viambata sumu na zilizoisha muda wa matumizi ambazo zilikamatwa kupitia ukaguzi maalumu uliofanyika katika maduka mbalimbali Kanda ya Ziwa.

Akizungumza Ijumaa Septemba 09, 2022 wakati wa zoezi la kuteketeza shehena hiyo lililofanyika katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza, Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Arnold Kubingwa amesema hatua hiyo inalenga kuondoa sokoni bidhaa zote zenye zisizofaa kwa matumizi kwani zina madhara kwa watumiaji.

Kubingwa ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa wanazoziagiza na kuziuza zinakidhi matakwa ya viwango ikiwemo kuangalia tarehe ya uzalishaji na mwisho wa matumizi.

Amesema TBS itaendelea kutoa elimu kwa jamii kutambua bidhaa zilizopigwa marufuku sokoni na kuwa na utamaduni wa kukagua bidhaa kabla ya matumizi na kwamba wafanyabiashara wanapaswa kuwa waaminifu kwa kuteketeza bidhaa zisizofaa.

“Wafanyabiashara wanapaswa kufuata matakwa ya Sheria katika utunzaji wa bidhaa zinazopaswa kuwa sokoni, uhifadhi wake wake katika maghala na uteketezaji wa bidhaa ambazo hazifai kuwa sokoni, wakishindwa kufanya hivyo tutaendelea kuziondoa na kuchukua hatua dhidi yao” amesema Kubingwa.

Naye Afisa Usalama wa Chakula TBS Kanda ya Ziwa, Elikaneny Minja amesema bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na ambazo zina viambata sumu ni hatari kwa afya ambapo zinaweza kusababisha maradhi ya ngozi ikiwemo kansa kwa watumiaji na  kwamba madhara hayo yanaweza kuhamia kwa watoto walio tumboni ikiwa mtumiaji ni mjamzito.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii kuzitambua bidhaa zilizopigwa marufuku na zenye viambata sumu, pia tumeziweka kwenye tovuti ya TBS ili wananchi wazitambue na kujiepusha na matumizi yake” amesema Minja na kuongeza kuwa TBS inashirikiana na maafisa afya na biashara katika ngazi za Halmashauri ili kufanya ukaguzi na kuondoa sokoni bidhaa zisizofaa.

Nao baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza akiwemo Happyness Enock pamoja na Amos Makinga wameipongeza TBS kwa jitihada za kuondoa sokoni bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambata sumu na kuongeza kuwa ni vyema wafanyabishara wanaokamatwa wakiuza bidhaa hizo wakachukuliwa hatua kali za kisheria.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa Arnold Kubingwa (kushoto) na Afisa Usalama wa Chakula TBS Kanda ya Ziwa, Elikaneny Minja (kulia) wakishuhudia shehena ya vipodozi na chakula ikiteketezwa katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza baada ya kuisha muda wa matumizi, na yenye viambata sumu.
Afisa Udhibiti Ubora TBS Kanda ya Ziwa, Arnold Kubingwa akizungumzia zoezi la kuteketeza bidhaa hizo ambazo kama zingekuwa halali zingekuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100.
Afisa Usalama wa Chakula TBS Kanda ya Ziwa, Elikaneny Minja (kulia) akizungumza na wanahabari wakazi wa zoezi la kuteketeza shehena hiyo.
Mkazi wa Jiji la Mwanza, Happyness Enock akizungumzia umuhimu wa kukamata na kuteketeza bidhaa zisizopaswa kuwa sokoni.
Mkazi wa Jiji la Mwanza, Amos Makinga akitoa pongezi kwa TBS kwa kukamata na kuteketeza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambata sumu kwa kuwa ni hatari kwa afya ya watumiaji.
Shehena ya vipodozi na chakula ikiteketezwa katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza.
Shehena ya vipodozi na chakula iliyoteketezwa na TBS katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza
Shehena ya vipodozi iliyoteketezwa na TBS katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza baada ya kuisha muda wa matumizi.
Shehena ya vipodozi na chakula iliyoteketezwa na TBS katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza baada ya kuisha muda wa matumizi.
Shehena ya vipodozi na chakula iliyoteketezwa na TBS katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza baada ya kuisha muda wa matumizi.
Shehena ya vipodozi na chakula iliyoteketezwa na TBS katika dampo la Buhongwa jijini Mwanza baada ya kuisha muda wa matumizi.

No comments:

Powered by Blogger.