LIVE STREAM ADS

Header Ads

Makamu wa Rais aagiza mradi wa maji Butimba Mwanza ukamilike mapema

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa chanzo na kituo cha tiba ya maji Butimba jijini Mwanza.

Akizungumza Jumatano Septemba 14, 2022 kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe hilo, Dkt. Mpango alisema maji ni uhai na hakuna kiumbe ambacho kinaweza kuishi bila maji hivyo kwa kulitambua hilo Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji ambapo dhamira ni kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana kila eneo ikiwa ni kutekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani.

Dkt.Mpango alisema mradi huo ulitakiwa ukamilike Feburuari 2023 lakini kutokana na changamoto ya uhaba wa maji amemuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha mradi huo unakamilika mwishoni mwa mwaka huu ili wananchi wa Nyamagana na Ilemela waweze kupata maji ya uhakika.

"Jana nilipokuwa nazindua kituo cha mabasi na malori Nyamhongolo, sauti za wananchi kuhitaji maji zilikuwa nyingi ndiyo maana nikamuagiza Waziri wa maji na timu yake wakae na Mkandarasi wafanye kazi usiku na mchana ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu kazi katika kutekeleza mradi huu ili kumaliza kabisa kero ya maji Mwanza" alisema Dkt.Mpango.

Dkt.Mpango alisema mradi huo utakapokamilika wananchi wanaoishi karibu na chanzo hicho wapewe kipaumbele kupata maji huku akitoa rai kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA) kutowabambikia wananchi bili za maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema atashirikiana na timu yake, Mkuu wa Mkoa Mwanza na Wakuu wa Wilaya wote kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili iwe zawadi ya Christmas kwa wana Mwanza.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga alisema unajengwa kwa fedha za mkopo wa mashariti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na European Investment Bank (EIB).
Alisema mradi huo hadi kukamilika utagharimu shilingi bilioni 69.3 na utazalisha lita za ujazo milioni 48 kwa siku ambapo utahudumia wakazi wapatao 450,000.

Mhandisi Sanga alisema Mradi huo umelenga kutatua changamoto ya maji katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Mwanza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alisema mradi huo utakapokamilika utakuwa ni suluhusho kubwa la changamoto ya maji kwa mji wa Mwanza na maeneo ya jirani. 
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Antony Sanga akitoa maelezo kuhusiana na ujenzi wa mradi wa maji Butimba jijini Mwanza.
Wakazi wa Jiji la Mwanza wakiwemo viongozi mbalimbali wa CCM wakiwa kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa chanzo cha maji Butimba unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA).
Mwonekano wa mradi wa chanzo cha maji kutoka Ziwa Victoria eneo la Butimba jijini Mwanza unaendelea kujengwa.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.