LIVE STREAM ADS

Header Ads

Makamu wa Rais azindua jengo la huduma za Saratani Hospitali ya Bugando, Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amezindua rasmi jengo la huduma za Saratani katika Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) jijini Mwanza, Jumanne Septemba 13, 2022.

Akizungumza baada ya kukagua na kuzindua jengo hilo, Dkt. Mpango alisema takwimu hapa nchini zinaonyesha kuwa watu elfu 42 hupata ugonjwa wa Saratani kila mwaka na kwamba kutokana na idadi hiyo Serikali imeamua kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huo na mengine yasiyoambukiza.

"Serikali imewekeza katika kutengeneza afua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, na miongoni mwa mikakati iliyopo ni pamoja na kupunguza vihatarishi vya magonjwa haya kwa kuelimisha jamii kuchukua hatua stahiki za kuboresha mtindo wa maisha kwa kuzingatia ulaji unaofaa, kupunguza matumizi ya pombe, kuacha matumizi ya tumbaku na kufanya mazoezi" alisema Dkt. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango alisema pamoja na kukamilika kwa jengo hilo, kuna baadhi ya huduma hazitaweza kutolewa kwa sasa kutokana na upungufu wa mashine za mionzi na kuagiza Wizara ya Afya kutatua changamoto hiyo.

"Natoa maelekezo kwa Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu) kwa mwaka huu wa fedha kupitia fedha za Global Fund kutoa bilioni 3.1 kwa ajili ya ununuzi wa mashine moja ya mionzi" aliagiza Dkt. Mpango.

Katika hatua nyingine Dkt. Mpango alitumia fursa hiyo kukemea baadhi ya tabia hatarishi zinazotajwa kusababisha maradhi ya kansa hususani katika ukanda wa Ziwa Victoria ambazo ni pamoja na njia haramu za uvuvi na uhifadhi wa mazao ya samaki ambapo amevitaka vyombo vya udhibiti kushughulikia suala hilo.
Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Kanda Bugando, Dkt. Fabiani Massaga alisema ujenzi wa jengo hilo la huduma za Saratani katika Hospitali hiyo ulianza Septemba Mosi mwaka 2020 ambapo hadi kukamilika umegharimu shilingi bilioni 5.6.

Dkt. Massaga alibainisha kuwa kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1.9 zilitoka Serikali Kuu kupitia Wizara ya Afya, shilingi bilioni 3.1 ni mchango wa Hospital ya Bugando kupitia mapato ya ndani, wafanyakazi shilingi milioni 250 huku wadau mbalimbali wakichangia shilingi milioni 400.

Alisema ukubwa wa jengo hilo ni mita za mraba 4,100 na lina ghorofa tatu ambapo litakuwa na manufaa ya makubwa ikiwemo kuongeza idadi ya wagonjwa watakaopata huduma, kupunguza vifo vitokanavyo na Saratani, kuongezeka kwa ubora wa huduma pamoja na kupunguza gharama kwa wagonjwa wakiwemo waliokuwa wakisafiri hadi jijini Dar es salaam kwa ajili ya matibabu.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Hospital ya Kanda Bugando, Renatus Nkwande alisema baada ya ujenzi wa jengo hilo kukamilika, changamoto iliyopo kwa sasa ni uhaba mashine mbalimbali za matibabu ya mionzi ambazo zinagharimu kiasi cha shilingi bilioni 14.

"Tunaiomba sana Serikali iendelee kutusaidia kupata mashine hizo hatua itakayosaidia kuboresha huduma za matibabu ya mionzi katika Hosptali yetu ya Bugando, kutuunga mkono kuwapeleka kwenye mafunzo ya mionzi wataalamu wengi zaidi watakaokidhi idadi ya wagonjwa tunaowapokea" aliomba Askofu Nkwande.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alitoa wito kwa taasisi mbalimbali za dini kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya mkoani Mwanza ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiwa na viongozi mbalimbali wakati akizindua jengo la huduma ya Saratani katika Hospitali ya Kanda Bugando.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Adam Malima.
Baada ya kuzindua jengo la huduma za Saratani katika Hospitali ya Kanda Bugando, Pia Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amezindua jengo la huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Mwanza Sekou Toure pamoja na stendi mpya ya mabasi Nyamhongolo iliyopo Manispaa ya Ilemela.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akizungumza baada ya kuzindua jengo la huduma za Saratani katika Hospitali ya Kanda Bugando.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango (kushoto) akisalimiana na viongozi wa dini.
Wananchi wakiwemo watumishi wa Hospitali ya Kanda Bugando wakiwa kwenye hafla hiyo.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.