LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waajiri wahimizwa kusaini mikataba na wafanyakazi wa nyumbani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani (WOTESAWA) limewahimiza waajiri kutambua umuhimu wa kusaini mikataba ya ajira na wafanyakazi wao wa nyumbani kwani inalinda maslahi ya pande zote mbili.

Rai hiyo imetolewa Alhamisi Septemba 08, 2022 na Meneja Nyumba Salama kutoka Shirika la WOTESAWA, Jaqueline Ngalo wakati wa kikao cha waalimu wakuu pamoja na maafisa elimu jijini Mwanza.

Katika kikao hicho, Ngalo amesema shirika la WOTESAWA limetumia fursa hiyo kugawa mikataba 72 ya ajira kwa waalimu ili wakaisome na kuielewa kabla ya kuridhia kuisani wakiwa na wafanyakazi wao wa nyumbani.

“Mkataba ni kielelezo muhimu cha mahusiano ya ajira baina ya mwajiri na mwajiriwa na unalinda makubaliano na maslahi baina ya pande zote mbili hata inapotokea changamoto inakuwa rahisi kuitatua” amesema Ngalo.

Ngalo amesema wafanyakazi wa nyumbani wasio na mikataba ya ajira wamekuwa ni wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili wa kimwili, kiakili na kiuchumi na hata wanaposhindwa kuelewana na waajiri wao wamekuwa wakifukuzwa bila kupata stahiki zao ikizingatiwa wengi wanatoka vijijini.

“Changamoto iliyopo ni baadhi ya waajiri pia kutokuwa tayari kusaidini mikataba ya ajira na wafanyakazi wao wa nyumbani, tunaendelea kukutana na makundi mbalimbali katika jamii ili kuwaelimisha na kuwahamasisha kutambua umuhimu wa mikataba hiyo na kuisaini” alieleza Ngalo.

Ngalo pia ameongeza kuwa shirika la WOTESAWA linaendelea kuwaelimisha waajiri kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambapo hairuhusiwi mtoto chini ya miaka 14 kuajiriwa huku mwenye miaka zaidi ya 14 akiruhusiwa kuajiriwa ajira rahisi zisizo na madhara katika makuzi yake.

“Kulingana na sheria, kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi wa nyumbani anayekaa kwa mwajiri mwenye kipato cha kawaida ni shilingi 40,000 kwa mwezi na shilingi 80,000 kwa ambaye hakai kwa mwajiri” amesema Ngalo na kuongeza;

“Kwa waajiri anayelipiwa mshahara wa mfanyakazi wa nyumbani na mwajiri wake kima cha chini cha mshahara ni shilingi 130,000 kwa mwezi na kwa mwajiri mwenye kipato cha juu, wafanyakazi wa Ubalozi na wafanyakazi wakubwa kima cha chini ni shilingi 150,000 kwa mwezi” alibainisha Ngalo.

Kwa upande wake Afisa Elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwl. Mussa Lambwe amewahimiza waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani wakiwemo waalimu kutowaajiri watoto ama wanafunzi na kukatisha ndoto zao kielimu na badala yake watoe ajira kwa waliohitimu masomo kwani wanakuwa na uwezo wa kutimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Nao baadhi ya waalimu jijini Mwanza akiwemo Mwl. Vivian Nyambui pamoja na Mwl. Ezekiel Ntibikeha wamekiri kutambua umuhimu wa kusaini mkata ya ajira na wafanyakazi wa nyumbani wakisema inasaidia kila mmoja kutimiza wajibu wake na kuondoa mivutano baina ya mwajiri na mwajiriwa. Katika kikao hicho waalimu 72 wamepokea mikataba

Kwa mwaka 2021, shirika la WOTESAWA kupitia mradi jumuishi wa kuwawezesha wafanyakazi wa nyumbani (Inclusive Child Domestic Workers Empowerment- Phase II) unaofadhiliwa na taasisi ya “Novo Foundation” lilifanikiwa kuwashawishi waajiri 90 jijini Mwanza kusaini mikataba ya ajira na wafanyakazi wao ambapo shirika hilo limekuwa likifanya ufuatiliaji wa karibu wa usimamizi wa mikataba hiyo.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Meneja Nyumba Salama kutoka Shirika la WOTESAWA, Jaqueline Ngalo akieleza namna shirika hilo limekuwa likiwahamasisha waajiri kutoa mikataba kwa wafanyakazi wa nyumbani.
Afisa Elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwl. Mussa Lambwe akitoa shukurani kwa shirika la WOTESAWA kutokana na linavyoshirikiana na kada ya waalimu kuimarisha ajira kwa wafanyakazi wa nyumbani.
Mwl. Vivian Nyambui akizungumzia umuhimu wa mikataba baina ya wajiri na wafanyakazi wa nyumbani.
Mwl. Ezekiel Ntibikeha akizungumza baada ya kupokea mkataba kutoka shirika la WOTESAWA kwa ajili ajili ya kuusaini na mfanyakazi wake wa nyumbani.
Mmoja wa waalimu waliopokea mkataba akiusoma kabla ya kuusaini na mfanyakazi wake wa nyumbani.
Viongozi mblimbali jijini Mwanza ambao ni waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani wakiwa kwenye kikao cha wadau wa elimu ambapo kupitia kikao hicho, shirika la WOTESAWA limegawa mikataba ya ajira kwa wadau hao na kuwahamasisha kuisaini na wafanyakazi wao wa nyumbani.
Wadau wa elimu wakiwa kwenye kikao hicho.
Maafisa Elimu na Waalimu Wakuu jijini Mwanza wakiwa kwenye kikao hicho.
Meneja Nyumba Salama kutoka Shirika la WOTESAWA, Jaqueline Ngalo (kulia) akiwa na Afisa Msimamizi wa Nyumba Salama (Makao) na Uwezeshaji, Shirika la WOTESAWA, Demitila Faustine (kushoto) wakati wa kikao hicho.

No comments:

Powered by Blogger.