LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la WOTESAWA lawanoa wadau wa kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Wadau kutoka mashirika (NGO's) matatu na vikundi (CBO's) tisa wakifuatilia mada kutoka kwa Mkufunzi, Barnaba Solo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kusaidia utetezi wa haki za wafanyakazi wa nyumbani yaliyoandaliwa na Shirika la WOTESAWA.
***

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani (WOTESAWA) limetoa mafunzo kwa viongozi wa mashirika matatu na vikundi tisa wanaojihusisha na utetezi wa haki za wafanyakazi wa nyumbani.

Mashirika hayo ni The Light For Domestic Workers kutoka Morogoro, Haki Sawa kutoka Musoma na Initiative For Domestic Workers kutoka Bagamoyo pamoja na vikundi mbalimbali ikiwemo umoja wa wafanyakazi wa nyumbani Kata ya Mkuyuni, Inuka mfanyakazi wa nyumbani, Sikika Sauti Yangu, Nishirikishe Group, Juhudi ya Mfanyakazi wa Nyumbani na Dadas Group.

Msimamizi wa Mradi wa Sauti Yetu, Nguzo ya Mabadiliko, Demitila Faustine alisema mafunzo hayo ya siku nne yalianza Jumanne Agosti 31, 2022 kwa ufadhili wa Shirika la Global Fund for Women kupitia mradi wa 'Wawezeshe Wafanyakazi wa Nyumbani, Tetea Haki Zao' na Shirika la Women Fund Tanzania kupitia mradi wa 'Sauti Yetu, Nguzo ya Mabadiliko' kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kusaidia kuhamsisha kazi zenye staha kwa wafanyakazi wa nyumbani nchini Tanzania.

"Katika mafunzo haya tumewajengea uwezo wa usimamizi wa fedha, usimamizi wa miradi, uongozi, namna bora ya uundaji wa vikundi, ufuatiliaji wa tathimini ya miradi, uandishi wa taarifa pamoja na elimu ya afya ya uzazi ili kuhakikisha mfanyakazi wa nyumbani anakuwa salama" alisema Faustine na kuongeza;

"Maeneo mengine waliyojifunza ni utawala, utafutaji rasilimali fedha, usimamizi wa miradi, utatuzi wa mashauri ya wafanyakazi wa nyumbani, utoaji rufaa, uchechemuzi (advocacy), mawasilino, ushirikiano pamoja na ubia na wadau. Pia kuunda na kuimarisha mtandao (tapo) wa pamoja utakaosaidia kuhamasisha upatikanaji wa haki za wafanyakazi wa nyumbani" alibainisha Faustine. 
Pia Faustine alisema katika kipindi cha utekelezaji wa miradi hiyo, watakuwa na ajenda isemayo 'Mlinde, Jilinde Mpatie Mkataba wa Ajira Mfanyakazi wako wa Nyumbani' kwa lengo la kuwahamasisha waajiri kutoa mikataba kwa wafanyakazi wao wa nyumbani hatua itakayosaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima baina yao.

"Pia tumelenga kuwahamasisha wafanyakazi wa nyumbani kutambua umuhimu wa kazi zao, kufanya kazi kwa bidii, kuthamini kazi yao na kujiheshimu ili waweze kujiletea mabadiliko yakiwemo ya kiuchumi" alisema Faustine.

Aidha Faustine alibainisha kuwa mradi wa 'Sauti Yetu, Nguzo ya Mabadiliko' utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Agosti 2022 huku mradi wa 'Wawezeshe Wafanyakazi wa Nyumbani, Tetea Haki Zao'  ukitekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2021. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la The Light For Domestic Workers (LDW) la Morogoro, Beatrice Johnson alisema mafunzo hayo yamewapa fursa ya kujuana na kubadilishana uzoefu hususani kwenye masuala mbalimbali ya uongozi hatua mbayo itasaidia kukuza mashirika yao.

Johnson alitoa wito kwa wafanyakazi wa nyumbani kutofumbia vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa na baadhi ya waajiri na badala yake watoe taarifa katika mamlaka mbalimbali ikiwemo Serikali za Mitaa kwa msaada zaidi.

Naye Mratibu wa Shirika la Haki Sawa kutoka Musoma mkoani Mara, Godwin Charles aliomba Serikali kuridhia mkataba wa kimataifa utakaowezesha kupitisha Sheria ya mfanyakazi wa nyumbani kuwa na haki ya lazima ya kupewa mkataba wa kazi na mwajiri wake.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo jijini Mwanza.
Afisa Mradi Shirika la WOTESAWA, Demitila Faustine akitoa ufafanuzi kuhusiana na mafunzo hayo.
Mratibu Shirika la Haki Sawa, Godwin Charles alieleza namna mafunzo hayo yatawasaidia kupaza sauti ili kuhamasisha kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani.
Mkurugenzi Shirika la The Light For Domestic Workers, Beatrice Johnson akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo.

No comments:

Powered by Blogger.