LIVE STREAM ADS

Header Ads

TBS yatoa mafunzo kwa Maafisa Biashara, Afya mkoani Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa biashara na maafisa afya wa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza pamoja na Halmashauri za Mkoa huo kuhusu Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia utekelezaji wa majukumu na ushirikiano baina ya TBS na Mamlaka za Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika Septemba 05, 2022 katika ukumbi wa TMDA Buzuruga jijini Mwanza na kujumuisha washiriki zaidi ya 20.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Athumani Yusuphu Ngenya, Mkurungenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika hilo Lazaro Msasalaga alisema mafunzo hayo yataongeza ufanisi mkubwa kwa maafisa hao katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema TBS inatambua umuhimu wa watumishi wa umma katika Halmashauri za Mikoa yote ya Tanzania hususani maafisa afya na biashara kuwa na mchango mkubwa katika kulinda ubora, usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi ili kulinda afya ya walaji pamoja na kuleta tija kwenye uchumi.

Msasalaga alisema TBS imekuwa ikifanya shughuli za ukaguzi na udhibiti kwa kushirikiana na watumishi kutoka katika Ofisi za Halmashauri akisema wana mchakato endelevu wa kuendesha mafunzo kwa watumishi wa OR-TAMISEMI.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Elikana Balandya, Katibu Tawala Msaidizi Kitengo cha Rasilimali Watu, Daniel Machunda aliwaasa maafisa hao kutotumia Kanuni na Sheria wanazopewa kama fimbo ya kuwachapia wananchi na badala yake wazitumie kwa ajili ya kuwaelimisha ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora na mlaji apate bidhaa ambazo hazitakuwa na madhara kiafya.

Naye Afisa Afya kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sophia kiluvya alisema mafunzo hayo yatawawezesha kutambua mbinu mbalimbali za kutambua bidhaa salama na kuondoa zilizopigwa marufuku katika soko.

Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Antony Esaya, alisema mafunzo hayo yamesaidia kupanua wigo kwa maafisa biashara na afya ngazi za Halmashauri itakayosaidia kuelimisha wananchi kuzalisha bidhaa bora na salama mkwa mtumiaji.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Daniel Machunda akifungua mafunzo ya Maafisa Biashara na Maafisa Afya kutoka Halmashauri za Mkoa Mwanza yaliyoandaliwa na TBS.
Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga (kushoto) akitoa salamu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TBS, Dkt. Athuman Ngenyo (hayuko pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa maafisa biashara na afya mkoani Mwanza. Wengine ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Daniel Machunda (katikati) pamoja na Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joseph Mwaipaja (kulia).
Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joseph Mwaipaja (kulia) akitoa salamu wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga pamoja na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Daniel Machunda
Maafisa Biashara na Maafisa Afya kutoka Halmashauri za Mkoa Mwanza pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza wakifuatilia mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mafunzo.
Washiriki wa mafunzo, viongozi wa TBS wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni.
Mafunzo ya aina hiyo pia yametolewa katika mikoa ya Pwani, Tanga na Mtwara ambapo litakuwa endelevu katika mikoa yote Tanzania Bara ambapo Maafisa Biashara na Maafisa Afya wa Halmashauri watasaidia katika shughuli za ukaguzi zinazofanywa na TBS, kusaidia ukuaji wa viwanda na biashara pamoja na kuondoa sokoni bidhaa zilizopigwa marufuku.

No comments:

Powered by Blogger.