MWANZA: TBS yawanoa maafisa kutoka maabara za ubora na uchunguzi kuhusu vipimo
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mhe. Amina Makilagi amefungua mafunzo kwa wafanyakazi kutoka maabara za ubora na uchunguzi kuhusu sayansi ya vipimo yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Mhe. Makilagi amefungua mafunzo hayo Jumanne Septemba 06, 2022 katika ukumbi wa TMDA Buzuruga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhe. Adam Malima.
Mhe. Makilagi ametumia fursa hiyo kuipongeza TBS kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatakuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika taasisi zinazofanya vipimo vya ubora na uchunguzi na kutoa majibu sahihi.
"Mwanza ni Mkoa wa kimkakati unaokua kwa kasi, tuna miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi na afya hivyo baada ya mafunzo haya tunategemea kuona mkifanya vipimo vitakavyotoa majibu sahihi na ya kuaminika" amesema Mhe. Makilagi.
Naye Mkurugenzi Mkuu TBS, Dkt. Athuman Ngenya amesema washiriki wa mafunzo hayo watajengewa uwezo kuhusu sayansi ya vipimo (Metrolojia) pamoja na mchakato wa kuangalia ubora wa bidhaa katika vipimo (Ugezi) kwani hizo ni nyenzo muhimu katika uzalishaji akisema "ukikosea vipimo hata bidhaa yako haiwezi kuwa na ubora".
Baadhi ya washiriki akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Mizani TANROADS Mkoa Mwanza, Mhandisi Joseph Kalala pamoja Mwakilishi wa Maabara ya SGS, Suma Mwakyembe wamesema mafunzo hayo ni muhimu na yatasaidia kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi zao.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi akifungua mafunzo kuhusu elimu ya Metrolojia kwa Wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za vipimo na uchunguzi mkoani Mwanza.
Katika mafunzo hayo, TBS pia imehimiza taasisi mbalimbali ikiwemo za uzalishaji, ujenzi na afya kuendelea kutumia Maabara ya Taifa ya Vipimo kwa ajili ya kupima vifaa vyao vya maabara na kupata leseni ya ubora.
No comments: