LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mwenyekiti wa CCM Nyamagana aonya uongozi wa kinafiki

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Peter Begga ameahidi kushirikiana na vyema na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza huku akionya kuwa hatavumilia uongozi wa kinafiki ambao unakwamisha shughuli za maendeleo.

Begga aliyasema hayo Oktoba 25, 2022 wakati akijitambulisha kwa wafanyakazi wa Halmashauri hiyo ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kuchanguliwa Oktoba Mosi mwaka huu katila nafasi hiyo.

Alisema watumishi wote ni wamoja na kwamba wanamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa sababu wanafanya kazi kwa niaba ya Serikali ambayo inaongozwa na CCM hivyo washirikiane kufanya kazi kwa weledi wa taaluma zao ili kutatua changamoto za wananchi.

“Mkifanya kazi vizuri na sisi chama tutafanya vizuri zaidi maana tumejipanga kuwahudumia watanzania na mimi sitapenda uenyekiti wa fitina fitina, kuletewa majungu majungu kwamba fulani kafanya hivi, sitakubali na ninachowasihi mfanye kazi kwa weledi kama mnavyojua CCM ndiyo msimamizi wa shughuli zote za maendeleo ambazo zinafanywa na Serikali” alisema.

“Tukipata tatizo sehemu hatutakuwa watu wa kukurupuka na kuisema idara flani, tutafuatilia kwa utaratibu maana tumejipanga kuwahudumia wananchi kwa haki na kwa kutatua changamoto zao, mimi kama mwenyekiti kijana siko tayari kuona ifikapo 2024 kwenye uchaguzi wa Wenyeviti wa Mtaa tunapoteza Mtaa hata mmoja maana tukitatua changamoto za wananchi na wao wataendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi” alisema Begga na kuongeza;

“Utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi Rais ni awamu mbili kwa hiyo wito wangu kwenu narudia tena ongezeni weledi mnapowahudumia wananchi ili itakapofika mwaka 2025 tukiwa tunamnadi mgombea wetu ambaye si mwingine bali ni Rais Samia Suluhu Hassan tusiwe na haja ya kujieleza, wananchi wawe wameona mambo mazuri aliyowafanyia ambayo ndiyo dhamira yake, sisi wasaidizi wake ndani ya chama tutayasimamia maelekezo yake na nyie wasaaididi wake upande wa Serikali yatekelezeni vizuri”alisema Begga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Yahaya Sekiete pamoja na Mstahiki Meya wa jiji hilo, Costantine Sima walisema ushirikiano uliopo baina ya CCCM na watumishi ni mzuri huku wakimwahidi Mwenyekiti huyo kuendelea kushirikiana naye ili kuleta maendeleo na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020/2025.
Na Clara Matimo, Mwanza
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Costantine Sima (katikati) akizungumza kwenye kikao hicho. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Yahaya Sekiete na kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Begga.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwa kwenye kikao hicho.

No comments:

Powered by Blogger.