LIVE STREAM ADS

Header Ads

Zaidi ya wasichana 1,000 wapata mafunzo Ilemela

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Sauti ya Wanawake Ukerewe (SAWAU) kwa kushirikiana na shirika la MIBOS limetoa mafunzo ya utambuzi na ujasiriamali kwa zaidi ya wasichana 1,000 katika Kata sita za Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la SAWAU, Sophia Donald aliyasema hayo Oktoba 11, 2022 wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyika wilayani Ilemela.

Alisema SAWAU kwa kushirikiana na MIBOS limefanikiwa kuwawasaidia wasichana kujitambua, kutambua haki zao na kujitegemea kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali kupitia mradi wa ‘Imarisha Wasichana’ unaofadhiliwa na shirika la kutetea haki za watoto (Children’s Rights & Violance Prevention Fund- CRVPF) la nchini Uganda.

“Tumewafikia wasichana zaidi ya elfu moja na kuwapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo afya ya uzazi na ujasiriamali ambapo katika mkataba mpya ujao tutaimarisha kile tulichokianzisha, tutawawezesha vyerehani ili kupitia vikundi vyao waanzishe shughuli za uzalishaji mali” alidokeza Donald.

Pia Donald alisema shirika hilo linaunga mkono mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili kuzuia mtoto mwenye umri chini ya miaka 14 kuolewa akisema wakati wa mabadiliko hayo kufanyika ni sasa.

Akisoma risala kwenye maadhimisho hayo, Shamira Valentino alisema mradi wa Imarisha Wasichana umewasaidia kutatua changamoto za mimba zinazowakabili wasichana ikiwemo mimba za utotoni, kupata sehemu salama ya kujadiliana masuala mbalimbali pamoja na kupata mafunzo yatakayowasaidia katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Baadhi ya wasichana kwenye maadhimisho hayo akiwemo Jackline Daniel, Frida Fladius na Anicia Juma walisema mradi wa Imarisha Wasichana umewasaidia wasichana walio shule na nje ya shule kukabiliana na vishawishi mbalimbali vinavyoweza kuhatarisha hatma ya maisha yao.

Mradi wa Imarisha Wasichana unatekelezwa wilayani Ilemela katika Kata sita za Nyakato, Kahama, Buswelu, Ibungilo, Kisenye na Nyasaka.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Shamira Valentino akisoma risala kwa niaba ya wasichana wenzake.
Wasichana wakionesha talanta ya kucheza.
Mkurugenzi Shirika la SAWAU, Sophia Donald (kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiri mbalimbali kwenye siku ya mtoto wa kike duniani.
Wasichana wajasiriamali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Wasichana wakiwa kwenye mavazi ya aina mbalimbali wakati wa onesho la mitindo kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani.
Wasichana wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Wasichana wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani 2022 jijini Mwanza.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani 2022 yaliambatana na kaulimbiu "Wakati Wetu ni Sasa, Haki Zetu, Hatma Yetu".
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.