LIVE STREAM ADS

Header Ads

Bodaboda watakiwa kuwa mabalozi wa kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Madereva wa bodaboda na bajaji mkoani Mwanza wametakiwa kuwa waaminifu kwa wateja wao na kuepuka tabia ya kujihusisha na matukio ya uhalifu kwa abiria wao hususani watoto na wanawake ambao wamekuwa wahanga zaidi.

Rai hiyo imetolewa Novemba 28, 2022 na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isaack Ndasa wakati akifungua kongamano la waendesha bodaboda na bajaji ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.

"Tupunguze unyanyasaji na ukatili tunapokuwa tunawasafirisha abiria hususani watoto na wanawake ambao ndio wateja wetu wakubwa, kumbuka ukimtendea ukatili mtoto wa mwenzio, wa wako pia hatakuwa salama maana ukatili huo utakurudia kwani ndivyo imani ndivyo ilivyo" amesema Ndasa.

Ndasa amebainisha kwamba kumekuwa na baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji wasio waadilifu ambao nyakati za alfajili ama usiku huwatendea vitendo vya ukatili ikiwemo wa kingono abiria wao hasa wanafunzi na akina mama wakati wanawahi au kutoka kwenye shughuli zao na hivyo kuwataka kuacha mara moja tabia hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Jamii Mkoa Mwanza, Dustan Kombe amewataka waendesha bodaboda na bajaji kujitambua na kuzingatia elimu wanayopewa ili kuwa sehemu ya kuimarisha usalama katika jamii.

"Acheni kuwatendea ukatili watoto, wateja wenu ambao huwaamini na kuwaagiza nyumbani kwao, pia msiwaamini watu msiowafahamu na kuwaachia bodaboda nyakati za usiku kwani hao ndio wanawaharibia sifa kwa kujihusisha na vitendo vya ukatili" amesema Kombe.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Jeshi la Polisi Mkoa Mwanza, Faraja Nkinga amefichua namna waendesha bodaboda na bajaji wanavyokengeuka na kujihusisha kimapenzi na wadada wa kazi ama mabinti katika familia nyingi pindi wanapoagizwa na wazazi ama walezi kupeleka mahitaji mbalimbali nyumbani.

"Unakuta bodaboda unamuamini, unamwagiza nyumbani kwako kila siku, unakuja kugundia amemgeuza mtoto wako kuwa mkewe. Acheni hiyo tabia maana hamtaepuka mkono wa Sheria" amesema Mkinga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea haki za watoto na wanawake la KIVULINI, Yassin Ally amesema elimu inayotolewa kwa waendesha bodaboda na bajaji itasaidia kuwaweka salama watoto na wanawake kwani kundi hilo limekuwa likichangia ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

"Kuna baadhi ya vituo vya bodaboda jijini Mwanza ikiwemo Mohammed vimegeuka vituo vya uporaji kwa abiria nyakati za usiku, naomba jeshi la polisi liongeze nguvu kuimarisha usalama kwenye vituo hivyo ikiwezekana ziundwe Kanda Maalum za kipolisi kwenye vituo hivyo" ameshauri Ally.

Ally ametoa rai pia kwa jamii kuwa kuzingatia malezi bora kwa watoto kwani takwimu za jeshi la polisi kuanzia mwezi Januari hadi Septemba zinaonyesha watoto 10,44 wamelawitiwa huku watoto wa kiume wakiwa waathirika zaidi (watoto 878) na wakike wakiwa ni 166.

Nao baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji jijini Mwanza akiwemo Paulo Bundala wameshauri abiria kubadilika na kuacha kuwatumia bodaboda wasio na vituo rasmi vya kazi kwani hao ndio wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu hususani nyakati za usiku

"Ukichukua bodaboda kwenye kituo, akikutendea ukatili ni rahisi kumpata na kumchukulia hatua za kisheria kwani tunafahamiana na vituo vyetu vimesajiliwa" amesema Bundala.

"Ukimuona mwenzako anajihusisha na vitendo vya ukatili, toa taarifa polisi ama kwenye chama na taarifa yako itakuwa siri, sheria itachukua mkondo wake, wale ambao hawajapa vitambulisho, wafike ofisini wasajili ili watambulike" amesisitiza Mwenyekiti wa bodaboda Kanda ya Mwanza Mjini, Ramadhan Kakuba.

Katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, elimu imeendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 10, 2022 ikiambatana na kaulimbiu isemayo "Kila Uhai una Thamani: Tokomeza Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto".
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isack Ndasa akifungua kongamano la bodaboda jijini Mwanza lenye lengo la kutoa elimu ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Bodaboda jijini Mwanza wakifuatilia kongamano hilo wakati Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isack Ndasa akizungumza.
Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Jamii Mkoa Mwanza, Dustan Kombe akitoa mada ya usalama kwa bodaboda wakati wa kongamano hilo.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye kongamano hilo.
Mwenyekiti wa bodaboda Kanda ya Mwanza Mjini, Ramadhan Kakuba akiwahimiza bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwa mabalozi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.
Dereva bodaboda jijini Mwanza, Paulo Bundala akizungumza kwenye kongamano hilo ambapo amewakemea bodaboda wasio waadilifu wanaochafua sekta hiyo.
Mwenyekiti kampeni ya kutokomeza ukatili katika jamii iitwayo Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa Mwanza, Gaston Didas akitoa rai kwa waendesha bodaboda kuwa mabalozi wa kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia. 
Viongozi wa jeshi la polisi mkoa Mwanza, Shirika la Kivulini na waendesha bodaboda wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Viongozi wa jeshi la polisi mkoa Mwanza, Shirika la Kivulini na waendesha bodaboda wakiwa kwenye picha ya pamoja.

No comments:

Powered by Blogger.