AZZA HILLAL AANZA RASMI KAZI ZA UBUNGE ITWANGI, AFANYA SHEREHE MASUNULA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza kwa njia ya Simu na Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad akila chakula cha pamoja na wananchi Jimbo la Itwangi
Na Kadama Malunde - Shinyanga
Kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi, Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, ameanza rasmi majukumu yake ya Kibunge kwa kuwatambua na kuwapongeza walimu, wanafunzi pamoja na jamii ya Masunula walioweka rekodi ya kihistoria ya ufaulu wa miaka tisa mfululizo katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba.
Hatua hiyo imekuja kufuatia matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba 2025, ambapo wanafunzi wote 30 wa Shule ya Msingi Masunula iliyopo Kata ya Usule, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wamefaulu kujiunga na masomo ya Kidato cha Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026.
Kati yao, wanafunzi 18 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za bweni huku wanafunzi 12 wakijiunga na shule za sekondari za kutwa, wote wakipata daraja la “A”.
Sherehe maalum ya pongezi imefanyika Jumatatu Januari 5, 2026, katika viwanja vya Shule ya Msingi Masunula na kuhudhuriwa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, madiwani wa kata za Jimbo la Itwangi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Edward Ngelela, viongozi wa CCM, wenyeviti wa vijiji, maafisa elimu kata, maafisa watendaji wa kata, wazazi, wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Azza amewapongeza walimu na wanafunzi kwa juhudi zao, akibainisha kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya nidhamu, bidii na mshikamano mkubwa kati ya walimu, wazazi, viongozi wa kijiji na wanafunzi.
“Heri ya Mwaka Mpya 2026! Leo Januari 5, 2026, nimeanza rasmi kazi ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Itwangi. Tumekuja hapa Masunula kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu, walimu waliofanya kazi kubwa na jamii yote kwa ushirikiano wao. Licha ya shule kuwa ya kijijini, imekuwa bingwa wa matokeo ya Darasa la Saba kwa miaka tisa mfululizo. Nimeona ni vyema tufurahi pamoja, tule pamoja na kujumuika pamoja,” amesema Mhe. Azza.
Katika hafla hiyo, Mhe. Azza amekabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu kwa walimu wa shule hiyo, zawadi kwa wanafunzi wote waliohitimu na kuchaguliwa kujiunga na sekondari, pamoja na kuwathamini wazazi, viongozi wa kata na kijiji kwa mchango wao mkubwa katika mafanikio ya shule hiyo.
Ameelza kuwa pongezi hizo haziendi mikono mitupu, bali anawapatia zawadi za bahasha kwa Walimu wote 10 wa shule hiyo, vikombe vyenye picha ya Mbunge vikiwa na maandishi ya kuwapongeza, na vikombe pia kwa Serikali ya Kijiji, huku kwa upande wa wanafunzi wote 30 amewapatia “Counter Books” 10 kwa kila mmoja.
Aidha, Mhe. Azza ameshiriki chakula cha pamoja na wananchi waliohudhuria hafla hiyo ikiwa ni ishara ya mshikamano na umoja.
Aidha, amesema mbali na pongezi na zawadi hizo, pia changamoto zote ambazo zinaikabili shule hiyo tayari ameshaziwalisha kwa Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe, ambaye pia alipiga simu kwenye hafla hiyo na kuipongeza shule, huku akiahidi kufanya ziara shuleni hapo na kwamba yale yote ambayo Mbunge Azza amemuambia juu ya shule hiyo watayafanyia kazi.
Pia ameahidi kuendelea kushirikiana na jamii ya Masunula na Serikali kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi wa Jimbo la Itwangi.
Amewataka Wazazi, Sungusungu, Serikali ya Kijiji, Kamati ya Shule, Viongozi wa Serikali, waendelee kuwa karibu na Walimu na kuzungumza lugha moja ili waendelee kufaulisha wanafunzi kwa ufaulu wa daraja “A” na kwamba shule zingine zinapaswa kuiga mfano huo wa Masunula.
“Shule hii ya Masunula na historia nayo nilishafika hapa mwaka 2017 nikiwa Mbunge wa Vitimaalum, nikiwa na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga kipindi hicho Jasinta Mboneko na ilikuwa inataka kufungwa sababu ya ukosefu wa choo, nikajenga choo kwa kushirikiana na nguvu za wananchi, hivyo changamoto zote tutazitatua kwa vitendo,” ameongeza Mhe. Azza.
“Nataka kuona Shule ya Msingi Masunula na shule zote ndani ya Jimbo la Itwangi zinafanya vizuri katika mitihani ya taifa. Kwa kuwa Masunula imeonesha mfano mzuri, hatuna budi kuja kujifunza hapa ili tuone wenzetu wamefanikiwaje,” amesema Azza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Mhe. Edward Ngelela ameipongeza Shule ya Msingi Masunula kwa kuwa mfano wa kuigwa, wakisisitiza umuhimu wa shule nyingine kuja kujifunza mbinu zilizowezesha mafanikio hayo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, ameipongeza shule hiyo kwa mafanikio ya kitaaluma, huku akiahidi kutuma timu ya wataalamu kufanya tathmini ya changamoto zake ili zitatuliwe.
Afisa Elimu wa Shule za Msingi wa halmashauri hiyo Andrew Mitumba, amesema Shule ya Msingi Masunula ni jicho la Halmashauri, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi na walimu uendelee.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Daudi Shineneko, akisoma taarifa ya shule, amesema ilianzishwa mwaka 1977 ikiwa na wanafunzi 80, lakini sasa hivi ina jumla ya wanafunzi 615, pamoja na Walimu 10, Walimu nane walioajiriwa na walimu wawili wa kujitolea.
Amesema shule hiyo imeanza kufanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba kuanzia mwaka 2015 na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kwa miaka 9 sasa, huku malengo yao yakiwa ni kushika nafasi ya kwanza kitaifa.
Amesema katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2025, wanafunzi wote 30 wamepata ufaulu wa Daraja “A”, na wanafunzi 18 wamechaguliwa kwenda shule maalumu za bweni, huku mafanikio hayo yakitokana na ushirikiano wa wazazi, kamati ya shule, sungusungu na viongozi wa serikali ya kijiji.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kufundisha kwa bidii pamoja na kufanya mitihani ya majaribio mara kwa mara.
Mmoja wa wanafunzi waliofaulu, Sato Salumu, amemshukuru Mbunge Azza kwa msaada wa vifaa vya shule, akisema nidhamu na kusikiliza walimu ndizo siri ya mafanikio yao.
Jamii ya Masunula imeiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa maji kupitia Ziwa Victoria au uchimbaji wa visima virefu ili kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali inayowaathiri katika masomo yao.
Shule ya Msingi Masunula ilianzishwa mwaka 1977 ikiwa na wanafunzi 80 pekee, lakini kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 615, wakiwemo wavulana 298 na wasichana 317.
Pamoja na mafanikio makubwa ya kitaaluma, shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa madarasa, upungufu wa walimu, nyumba na vyoo vya walimu, ukosefu wa mabweni, uchakavu wa madarasa, ukosefu wa umeme, vifaa vya michezo pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad akizungumza


























No comments: