LIVE STREAM ADS

Header Ads

Shirika la KIVULINI laendesha kongamano la wanawake wilayani Ilemela

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Changamoto ya ukosefu wa malezi bora katika jamii imetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea ongezeko la vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo ulawiti, ubakaji pamoja na mimba kwa wanafunzi.

Hayo yameelezwa Disemba 02, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake la KIVULINI, Yassin Ally wakati akizungumza kwenye kongamano la kuwajengea uelewa wanawake wilayani Ilemela ili kutonyamazia matukio ya ukatili katika jamii.

Ally amesema imefika hatua wazazi hawana muda wa kufuatilia mienendo ya watoto wao, wako bize na masisha lakini si kuwakagua watoto wanapoenda ama kutoka shuleni kiasi kwamba wanashindwa kutambua mapema pindi wanapotendewa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Unakuta mtoto amelawitiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini baba hajui, mama hajui hadi unakuja kuambiwa na majirani. Hakikisheni mnafuatilia miendeno ya watoto wetu kuanzia sasa” amesisitiza Ally.

Ameongeza kuwa watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa vitendo vya ubakaji na ulawiti ambapo takwimu za jeshi la polisi zinaonyesha kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, watoto 1,044 wamelawitiwa, watoto 4,797 wamebakwa huku 1,115 wakipewa mimba hivyo takwimu hizo ziwe changamoto kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, wanaharakati na Serikali kuongeza jitihada za kuwalinda watoto.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isack Ndasa ameitaka jamii kuwa makini na suala la malezi vinginevyo jitihada za kimaendeleo zinazofanyika hazitakuwa na maana ikiwa jamii haitakuwa salama.

“Tuondoe hali ya kuona vitendo vya ukatili wa kijinsia kama mambo ya kawaida, vinginevyo tutajenga shule lakini tutasomesha mashoja, tutajenga hospitali lakini watakaoenda kutibiwa huko ni watoto waliobakwa na kulawitiwa. Lazima tuhakikishe hatufiki huko hivyo kila mmoja akitoka hapa akafuatilie malezi ya mtoto wake” amesisitiza Ndasa.

Nao baadhi ya wanawake walioshiriki kongamano hilo akiwemo Latifa Vicenti wamesema changamoto ya watoto kukosa malezi ya wazazi wote wa kiume na kike ni miongoni mwa sababu inayochochea watoto kuwa katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ubakaji na ulawiti na hivyo kuhimiza wazazi kila mmoja kutimiza wajibu wake.

Kongamano hilo limeandaliwa na shirika la KIVULINI ili kuwajengea uelewa kuhusu mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili duniani yaliyoanza Novemba 25 hadi Disemba 10, 2022.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye kongamano la wanawake wilayani Ilemela kwa lengo la kuwajengea uelewa kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isack Ndasa akizungumza kwenye kongamano la wanawake Wilaya ya Ilemela lililoandaliwa na Shirika la KIVULINI ikiwa ni sehemu yakuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isack Ndasa akizungumza kwenye kongamano hilo.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Latifa Vicent akichangia mada.
Mmoja wa wanawake walioshiriki kongamano hilo akichangia hoja kuhusu jitihada za kuchukua ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Wanawake wilayani Ilmeela wakifuatilia kongamano hilo.

No comments:

Powered by Blogger.