LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watu sita mbaroni kwa tuhuma za mauaji, kufukua makaburi wilayani Manyoni

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stellah Mutahibirwa.

Na Dotto Mwaibale, Singida 

WATU sita wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya mauaji ya watu, kufukua makaburi wilayani Manyoni na kuchukua sehemu za siri za miwili ya watu waliozikwa kwa ajili ya kutengeneza dawa ya kupata utajiri kuwauzia wateja wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, katika taarifa yake Jana kwa vyombo habari, alisema watuhumiwa hao ambao hakuwataja majina kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea, walikamatwa kufuatia msako uliofanywa na jeshi hilo kuanzia Machi 16 hadi 24 mwaka huu katika maeneo mbalimbali wilayani Manyoni na vijiji jirani vya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.

Alisema watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na kuhojiwa walikiri kuhusika na mauaji ya mtu mmoja mwanaume ambaye hajafahamika jina lake mwenye umri kati ya miaka 40 na 45 yaliyotokea Machi 3 mwaka huu eneo la relini Manyoni huku kifo chake ikisadikiwa kilitokana na kukanyagwa na treni kichwani na mguu wa kushoto.

Kamanda Mutabihirwa alisema baadhi ya viungo vya mtu huyo vilikuwa pembeni ya kiwiliwili katika njia ya treni huku viungo vya sehemu y Siri vikiwa vimenyofolewa.

"Tulivyowahoji watuhumiwa walikiri kuhusika na tukio hilo na kueleza kwamba walikata sehemu za siri kama nywele,kuchapa na ulimi kwa lengo la kutengeneza dawa ili kuwapatia wateja wao wanaohitaji utajiri," alisema.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao pia wamekiri kujihusisha na vitendo vya kufukua makaburi wilayani Manyoni na kuua watu kwa lengo la kupata sehemu za viungo vya binadamu kwa ajili ya kutengeneza dawa ya kupata utajiri.

"Katika kukamilisha upelelezi wetu Jeshi la Polisi lilifanya upekuzi katika nyumba ya mtuhumiwa mmoja wao na kufanikiwa kukuta suruali moja nyeusi ya marehemu aliyeuawa Machi 3, 2023,vibuyu viwili vyenye shanga, kibuyu kimoja chenye ngozi ya kondoo," alisema.

Kamanda Mutabihirwa alisema vitu vingine vilivyokamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni pembe ya kondoo yenye kioo na shanga,pembe ya ng'ombe yenye vipembe viwili vidogo,vipande vitatu vya sanda,kaniki vipande viwili,kitambaa kimoja chekundu na kopo la mafuta yenye mchanga wa kaburi na nywele.

Kufuatia hali hiyo,Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limetoa wito kwa wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina na badala yake wafanye kazi kwa bidii kupata utajiri halali.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza na wananchi wilayani Manyoni alisema  kamati ya kuchunguza mauaji mfululizo ya watu yanayotokea wilayani Manyoni imefanikiwa kukamata watu wanaojihusisha na matukio hayo ambao wamekutwa na damu, viungo vya binadamu na nywele majumbani mwao. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza jana na wananchi wakati wa kuwasilisha ripoti ya kamati ya migogoro ya viwanja, alisema kamati ya kuchunguza mauaji ya watu wilayani Manyoni ambayo bado  inaendelea na kazi imeanza kuleta matunda ambapo watu kadhaa wamekamatwa.

"Hapa Manyoni tuliunda Kamati tatu ikiwamo ya kuchunguza mauaji ya watu Manyoni,ripoti ya awali ya mauaji imeanza kuleta matunda,kuna watu tayari tumewakamata tumewakuta nyumbani kwao wana damu,wana viungo vya binadamu na wana nywele na tayari wapo mikono ya sheria," alisema.

Serukamba ambaye hata hivyo hajutaja idadi ya watu waliokamatwa wakihusika na mauaji hayo,alisema waliokamatwa wamemtaja mganga mmoja wa kienyeji kwamba ndiye alikuwa anawatuma.

Mkuu wa Mkoa wa Singida aliunda Kamati ya Kuchunguza Mauaji ya watu Manyoni hiyo Januari 21, mwaka huu wakati akisikiliza kero  ambapo wananchi walipaza sauti kumuomba aingilie kati jambo hilo.

Katika hali ya kushangaza,wananchi hao walimweleza kuwa  mauji ya watu ambayo yameibua hofu kubwa kwa jamii baadhi ya pikipiki zinazomilikiwa na baadhi ya watumishi kwa ajili kuendesha biashara zao ndizo zinatumika kwenye mauaji hayo.


No comments:

Powered by Blogger.