LIVE STREAM ADS

Header Ads

BAKWATA Mwanza waadhimisha Siku ya Familia Duniani, watoka na maazimio 19

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa Mwanza limeadhimisha Siku ya Familia Duniani kwa kuandaa kongamano lililowashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo waumini wa dini ya kiislamu ili kujadili hatua za kuchukulia kulinda maadili mema katika jamii.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika Jumatatu Mei 15, 2023 katika Msikiti wa Mbugani, Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke alisema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mufti wa Tanzania pamoja na Serikali kuimarisha maadili katika jamii.

Sheikh Kabeke alisema suala la maadili ni muhimu katika jamii hivyo BAKWATA Mkoa Mwanza inatarajia kuzindua kampeni ya Mkuu wa Familia Ongea na Familia ili kuhamasisha wanafamilia wakiongozwa na mkuu wa Kaya kuwa na siku maalumu ya kuongea na familia ili kubaini changamoto mbalimbali ikiwemo za vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na kuzishughulikia lakini pia itasaidia kuimarisha upendo katika familia.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Watoto na Wanawake KIVULINI, Yassin Ally akiwasilisha mada kuhusu ukatili wa kijinsia kwenye maadhimisho hayo alisema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuelimisha jamii na kurejesheja maadili ambayo kwa siku za hivi karibuni yameonekana kumomonyoka na matumio ya ukatili ikiwemo ubakaji, ulawiti na mimba kwa wanafunzi yakiongezeka.

"Takwimu zilizotolewa na mwaka jana 2022 na jeshi la polisi zilionyesha kulikuwa na mashauri 1,044 ya ulawiti wa watoto kote nchini ambapo wasichana ni 166 na wavulana ni 878, tuliwekeza nguvu kumlinda mtoto wa kike tukidhani hayuko salama kumbe kwa takwimu hizi hata watoto wa kiume hawako salama hivyo tuongeze nguvu kuwalinda watoto wote ambapo wajibu huo unaanzia ngazi ya familia" alisema Ally.

Kaulimbiu ya Siku ya Familia Duniani 2023 ni "Imarisha Maadili na Upendo kwa Familia Imara"
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke akizungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yaliyofanyika Mei 15, 2023 katika Msikiti wa Mbugani jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Watoto na Wanawake KIVULINI, Yassin Ally akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo.
Washiriki wakifuatilia kongamano la Siku ya Familia Duniani lililoandaliwa na BAKWATA Mkoa Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Watoto na Wanawake KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akizungumza kwenye kongamano hilo.
Sheikh Msafiri Kitumbo akichangia hoja wakati wa kongamano la Siku ya Familia Duniani lililoandaliwa na BAKWATA Mkoa Mwanza.
Washiriki wakifuatilia kongamano hilo.
Waumini wa dini ya kiislamu wakifuatilia kongamano la Siku ya Familia Duniani lililoandaliwa na BAKWATA mkoani Mwanza, Jumatatu Mei 15, 2023.
Maazimio mbalimbali yaliafikiwa kwenye kongamano hilo kwa ajili ya utekelezaji.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.