LIVE STREAM ADS

Header Ads

Rais Samia apongeza ujenzi wa jengo la Hotel ya Nyota Tano jijini Mwanza "hongereni, kitu kizuri"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com  
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza mara baada ya kupokea maelezo kuhusu ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambapo alipongeza NSSF kwa mradi wa hoteli hiyo.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu (kushoto) akitoa maelezo kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu taratibu za kupitisha miradi mbalimbali ambayo hupitia Benki kuu ya Tanzania (BOT) ili ishauri na ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia na kuwa lengo kuu la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuwekeza kulinda fedha za mifuko.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF) Masha Mshomba, akitoa maelezo kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu ujenzi wa mradi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na NSSF iliyopo jijini Mwanza, ambapo alisema ujenzi huo unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Juni 2024 baada ya kupatikana muendeshaji wa hoteli mwishoni mwa mwezi huu.
Meneja Usimamizi wa Miradi NSSF, Mhandisi Helmes Pantaleo akitoa maelezo kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania namna mradi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano utakavyokuwa. Mradi huo una ghorofa 16, vyumba 168 vya kulala vya aina mbalimbali ikijumuisha sehemu ya kupumzikia Rais (Presidential Suite), migahawa, sehemu za vinywaji na michezo (sports bar).

Na Mwandishi wetu, Mwanza
Ni kauli iliyotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano inayomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi wa Jamii (NSSF).

“Hongereni sana kwa kweli ni kitu kizuri " Amesema Mhe. Rais Dkt. Samia. Katika ziara hiyo Mhe. Rais Dkt. Samia ametembelea mradi huo uliopo eneo la Capripoint jijini Mwanza tarehe 14 Juni 2023, akiwa amefuatana na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi.

Alisema baada ya kupata maelezo ya mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na kwa Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Helmes Pantaleo hana mashaka kuhusu mradi huo kwani wataalamu watakuwa wameshapiga mahesabu.

Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema vitega uchumi vya aina hiyo vitaongeza tija kwenye Mfuko huku akiwasisitiza wafanyakazi kuendelea kutoa huduma bora na kuacha tamaa wanapotekeleza majukumu yao.

Alisema Mfuko ukipata mapato mazuri zaidi uangalie kuwekeza kwenye maeneo mengine ikiwemo mkoani Dodoma na Dar es Salaam.

“NSSF sasa hii sio fedha yenu ni fedha za wafanyakazi huko nje, mko pale nendeni toeni huduma, ichungeni hiyo fedha ya wafanyakazi ili anapostaafu mtu baada ya utumishi wake akute mzigo wake,” alisema.

Kwa upande wake, Mhe. Patrobas Katambi alisema miradi ya aina hiyo ili ipitishe ni lazima Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ishauri na Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia na kuwa lengo kubwa la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza ni kulinda fedha za Mifuko.

Mhe. Katambi alisema maelekezo ya Rais yamesaidia kuhakikisha Mfuko unakuwa imara na wanandelea kuusimamia ambapo hivi sasa mabadiliko ni makubwa.

Akitoa maelezo kuhusu mradi huo wa hoteli, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alisema ujenzi wa hoteli hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2024 ambapo itachangia shughuli za uchumi za jiji la Mwanza.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa hoteli hiyo ni vema kukaenda sambamba na kuendeleza uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa sababu watu mbalimbali watakaokuja kwa shughuli za utalii watahitaji kulala katika hoteli hiyo.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia umbali kutoka hapa Mwanza kwenda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni kilimota 140 tofauti na kupitia Arusha ambako ni mbali, kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege Mwanza kutachangia na kuvutia watalii hivyo tunakuomba uwanja ule uendelezwe kwa viwango vya kimataifa,” alisema.

Mshomba alisema mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwaka 2016, lakini ilishindikana kutokana na changamoto ya kukosekana kwa muendeshaji wa hoteli, lakini mwaka 2017/18 walitangaza zabuni ya muendesha hoteli hata hivyo hakupatikana kutokana na mazingira ya kipindi hicho na mwaka 2019 pia ilishindikana kutokana na na janga la COVID. Mwaka huo huo 2019 mwezi Septemba walienda nchini Zambia na Afrika Kusini ili kupata uzoefu jinsi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya nchi hizo inavyopata waendeshaji wa hoteli ambapo NSSF ilipata kampuni ya Hilton Hotels Worldwide, Radissons Hotels na Legacy Hotel.

Akitoa maelezo ya hoteli hiyo, Mhandisi Helmes Pantaleo ambaye ni Meneja Usimamizi wa Miradi wa NSSF, alisema hoteli ina umla ya ghorofa 16, vyumba 168 vya kulala vya aina mbalimbali ikijumuisha sehemu ya kupumzikia Rais (Presidential Suite), migahawa, sehemu za vinywaji na michezo (sports bar).

Pia, kuna ukumbi mkubwa wa mikutano wa kuchukua watu 500, kumbi ndogondogo za mikutano, bwawa la kuogelea, sehemu za kufanyia mazoezi, ofisi, maduka, sehemu ya maegesho ya magari na juu kabisa ya jengo hili kuna sehemu ya kutua chopa (helkopta).
Tazama picha hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.